Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

UTATA KATIKA TUNGO

Nini maana ya Utata?

Utata ni hali ya tungo kuwa na maana zaidi ya moja. Neno au sentensi yenye utata hutatanisha kimaana yaani haieleweki kwa yakini humaanisha hivi au vile? Tazama mifano hapo chini;

 • Nenda ukanichukulie mbuzi.

Swali: Mbuzi mnyama au mbuzi kifaa cha kukunia nazi?

 • Juma anapanda.

Swali: Juma anakwea au anaotesha mbegu?

 • Ile nyumba ni ya wageni

Swali: Ni nyumba ya kulala wageni au nyumba inamilikiwa na wageni?

 • Mtoto amelalia uji.

Swali: Amelala juu ya uji au hakula kitu kingine zaidi ya uji kisha akalala?

 • Mwajuma ametumwa na Rama.

Swali: Aliyemtuma Mwajuma ni Rama au Mwajuma na Rama wametumwa?

Sababu za Kutokea kwa Utata

 1. Neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja.

Matumizi ya neno au sentensi yenye maana za moja huleta utata. Maneno yenye utata ni kama vile; panda, mto, kaa, ua, vua, mbuzi na mengine mengi yenye maana zaidi ya moja.

 • Matumizi ya lugha ya picha

Lugha ya picha huleta utata hasa hasa matumizi ya nahau. Kwa mfano sentensi; mwanangu amevaa miwani, inaweza kumaanisha amevaa vioo vya machoni au amelewa?

 • Matumizi ya kauli ya utendea

Kauli ya utendea mara nyingi hutatiza kwani huibua maana zaidi ya moja. Kwa mfano sentensi, Julia amempigia Asha ngoma. Hii inaweza kumaanisha ama Julia amempiga Asha kwa kutumia ngoma au Julia amepiga ngoma badala ya Asha.

 • Kutokuzingatia taratibu za uandishi

Katika uandishi maana huweza kugeuzwa endapo taratibu hazikuzingatiwa ipaswavyo. Tazama sentensi hapo chini;

 1. Baba Alika amerudi usiku sana.
 2. Baba, Alika amerudi usiku sana.

Endapo mwandishi alitaka kutoa ujumbe unaopatikana katika sentensi ya pili lakini akaandika kama ilivyoandikwa sentensi ya kwanza kutakuwa na utata.

 • Kutokuzingatia muktadha wa mazungumzo

Pia utata huweza kutokea endapo msikilizaji hatazingatia muktadha wa mazungumzo. Kwa mfano sentensi; Rama ametumwa na Asha dukani. Huweza kuleta utata kama msikilizaji hakuzingatia taarifa inayotolewa ni ya nani? Asha au Rama?  

 • Matumizi ya nafsi hasa ya umiliki.

Matumizi ya nafsi huweza kuleta utata endapo jina zaidi ya moja pamoja na nafsi ya umiliki itapotajwa. Kwa mfano sentensi; Zebeda alimuona Husna anaenda sokono na rafiki yake.

Swali: Je, rafiki ni wa Husna au Zubeda?

Jinsi ya Kuondoa Utata

Tunaweza kuondoa utata katika tungo kwa kuepuka mambo yote yanayopelekea utata kama ifuatavyo;

 1. Kutotumia neno au sentensi yenye maana zaidi ya moja.
 2. Kutotumia lugha ya picha.
 3. Kutotumia kauli ya utendea.
 4. Kuzingatia taratibu za uandishi.
 5. Kuzingatia muktadha wa mazungumzo.
 6. Kutokumia nafsi badala yake tutaje kwa urefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *