Monday, January 25Kiswahili kitukuzwe!

Mjengo wa Tungo

Karibu tena katika makala zetu zinazojikita katika kutoa maarifa ya kiswahili kwa kidato cha tatu. Leo tutajadili kuhusu namna tungo zinavyojengwa katika lugha.

Tungo ni nini?

Tungo ni kipashio cha kimuundo ambacho hutokana na uwekwaji pamoja wa vipashio vidogo ili kuunda kipashio kikubwa zaidi. Tungo huweza kutoa taarifa kamili au isiyo kamili.

Kimuundo kuna aina nne za tungo ambazo ni; tungo neno, tungo kirai, tungo kishazi na tungo sentensi. Mpangilio huu umeanza na tungo ya chini kabisa hadi tungo ya juu kabisa. Hivyo, neno hujenga kirai, kirai hujenga kishazi na kishazi hujenga sentensi. Angalia zaidi ufafanuzi hapo chini.

Tungo Neno

Neno ni kipashio kidogo kabisa cha kimuundo kilichoachiwa nafasi pande zote mbili na hutoa maana. Katika Kiswahili kuna aina mbalimbali za maneno kama ifuatavyo;

 • Nomino
 • Kivumishi
 • Kitenzi
 • Kielezi
 • Kiwakilishi
 • Kihisishi/Viigizi
 • Kiunganishi na
 • Kihusishi (http://www.kiswahilipedia.org/2019/10/vihusishi-vya-kiswahili-sanifu/)

Rejelea aina za maneno katika kiswahilipedia.org http://www.kiswahilipedia.org/2019/10/viunganishi-vya-kiswahili-sanifu/ http://www.kiswahilipedia.org/2019/10/vihusishi-vya-kiswahili-sanifu/

Tungo Kirai

Kirai ni kipashio cha kimuundo ambacho hujengwa na neno moja au zaidi. Kipashio hiki hujengwa na aina kuu za maneno, aina hizo ni; nomino, kivumishi, kitenzi, kielezi na kihusishi.   Kutokana na hilo tunapata aina tano za virai ambazo ni; Kirai Nomino, Kirai Kivumishi, Kirai Kitenzi, Kirai Kielezi na Kirai Kihusishi.

Kirai Nomino (KN)

Hii ni aina ya kirai ambayo hujengwa na nomino kama neno kuu. Aina nyingine za maneno husaidia kutoa ufafanuzi tu. Kwa mfano hapo chini, maneno yaliyoandikwa kwa herufi kozwa na mlalo ni Kirai Nomino.

 • Mtoto anacheza
 • Kijana shupavu ameogelea ziwani.                
 • Andazi limeungua mno.
 • Gari lililobeba magunia, limeelekea mashineni.
 • Wanafunzi wa kidato cha tatu, watafanya mtihani kesho.

Vijenzi vya Kirai Nomino

Kutokana na mifano hiyo, tuangalie vijenzi vya Kirai Nomino hapo chini.

1. Nomino pekee

Juma anakula chenza.

Mariamu ni msumbufu.

Viazi huokoa muda.

2. Nomino na Kivumishi

Mtoto mzuri anacheza ngoma ya asili.

Mwalimu wetu hashindwi maswali.

Kijana mpole atapata nafasi.

3. Nomino, kiunganishi na nomino nyingine

Baba na mama wanalima.

Wavulana na wasichana hufanya kazi kwa bidii.

Koti na tai ni unadhifu.

Tulikula wali na nyama.

4. Nomino na Kishazi tegemezi kivumishi (βv)

Mtoto aliyekula viazi, hajala wali.

Ng’ombe aliyenenepeshwa, ameuzwa kwa bei kubwa.

Mama anayeumwa, amepelekwa hospitali.

Kiti kilichovunjika, kimetupwa.

5. Kiwakilishi pekee

Yeye ni msomi.

Kwao ni mbali sana.

Chagua hii achana na ile.

6. Kiwakilishi, kiunganishi na kiwakilishi kingine

Yule na wao walishirikiana.

Yeye na mimi hatukuingia.

Wanafunzi wangu ni huyu na yule.

7. Kiwakilishi kiunganishi na nomino

Huyo na Jamila ni watoto wa mama mmoja.

Hicho na sahani havifanani.

8. Kiwakilishi na kivumishi

Huyo mrefu apite mbele.

Kile cha kijani hakiuziki.

Hawa wakorofi lazima waadhibiwe.

9. Kiwakilishi na Kishazi tegemezi kivumishi (βv)

Hiki kilichofunuliwa, ni maagano.

Wale waliofukuzwa kazi, wametajirika.

Vile vilivyochaguliwa, havifai tena.

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi kozwa na mlalo ni kirai nomino.

Kirai Kivumishi (KV)

Hii ni aina ya kirai ambayo hujengwa na kivumishi kama neno kuu. Kwa kuwa kivumishi hueleza sifa ya nomino mara nyingine kirai kivumishi hutokea ndani ya kirai nomino. Tazama mifano ya KV hapo chini.

 • Mtoto mvivu hapendi kazi.
 • Huyu ni mrefu.
 • Kijana hodari ameajiri wenzie.
 • Gari lililopakwa rangi mpya, limeanza safari.
 • Hatununui viatu vyeusi.    

Katika mifano hapo juu, maneno yaliyoandikwa kwa herufi kozwa na mlalo ni kirai kivumishi. Pia, kirai kivumishi hujumuisha kishazi tegemezi kivumishi (βv).

Kirai Tenzi (KT)  

Hii ni aina ya kirai ambayo hujengwa na kitenzi kama neno kuu. Kirai hiki ndicho kinachotoa taarifa kamili katika sentensi. Kwa sababu hiyo huwa kina hadhi sawa na kishazi na zaidi ya hapo kina hadhi sawa na sentensi. Tazama mifano hapo chini.

 • Juma anakimbia.
 • Mwalimu alikuwa anafundisha darasa lingine.
 • Popo ni mamalia.
 • Hapo ndipo penyewe
 • Kijana aliyepotea, ameonekana msituni.

Vijenzi vya Kirai Tenzi

Kirai kitenzi kinajengwa na viambajengo mbalimbali kama ifuavyo;

Kitenzi Kikuu pekee. Kwa mfano;

 1. Mtoto analia.

2. Meza imeanguka.

3. Kiti kimepakwa rangi.

Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu. Kwa mfano;

 1. Mwinyi alikuwa anapanda mlimani.

2. Msichana alitaka kujifunza ubaharia.

Kitenzi kishirikishi

 1. Hicho ndicho chenyewe.

2. Uvivu ni umasikini.

Kitenzi na kirai nomino

 1. Mwanafunzi anakula chungwa.

2. Gari limebeba mzigo.

3. Kiatu kimefungwa gidamu.

Kitenzi na kirai kielezi

 1. Anatembea harakaharaka.

2. Manamba wanalima shambani.

3. Treni litaondoka asubuhi sana.

Kitenzi na kirai kuhusishi

 1. Amekimbilia kwa mama yake.

2. Hiki ni cha kwake.

3. Amekula kwa kijiko.

Kirai Kielezi (KE)

Hii ni aina ya kirai ambayo imejengwa na kielezi kama neno kuu. Kirai hiki hutoa taarifa zaidi kuhusu tendo. Maranyingine hutokea ndani ya kirai tenzi. Tazama mifano ifuatayo;

 • Alikuja asubuhi.
 • Amekaa sakafuni.
 • Tunakutana mara kwa mara.

Kirai Kihusishi (KH)

Ni aina ya kirai inayojengwa na kihusishi kama neno kuu. Sehemu nyingine wanaita kirai kirai kiunganishi. Hata hivyo, kirai kiunganishi kinachotajwa kinapewa dhima ya kirai kihusishi. Na hii inatokana na kuwa kihusishi hakitajwi kama aina ya neno tangu mwanzo. Tazama mifano ya kirai kihusishi katika hapo chini.

 • Kijana alikuja kwa basi.
 • Mwanafunzi alienda kwa babu yake.
 • Yeye alipita kwa kasi.

Tungo Kishazi

Hii ni aina ya tungo inayoundwa na kirai kimoja au zaidi. Tungo hii huweza kutoa taarifa kamili au isiyo kamili. Taarifa kamili huwezeshwa na kitenzi kinachopatikana kwenye tungo hii.

Aina za Kishazi

Kishazi Huru

Kishazi hiki kimejengwa na kitenzi. Kwa hiyo hutoa taarifa kamili. Pia, Kishazi hiki kina hadhi sawa na sentensi. Tazama mifano hapo chini;

 • Kipindi kimeanza.
 • Kiatu kimevaliwa.
 • Samaki anaogelea majini.

Kishazi Tegemezi

Kishazi hiki kimejengwa na kitenzi kilichoshushwa hadhi kwa kuwekewa urejeshi. Kutokana na hilo, kishazi tegemezi hakiwezi kutoa taarifa kamili. Kwa mfano;

 • Mtoto aliyelazwa hospitali ya wilaya,
 • Mchezaji aliyepewa tuzo,
 • Mlango ulioharibika,

Kishazi tegemezi huweza kutokea mwanzoni mwa sentensi au mwishoni mwa sentensi. Pia, kishazi tegemezi ndicho kinachojenga sentensi changamani. Yaani bila kishazi tegemezi hakuna sentensi changamani.

Mifano Zaidi kuhusu kishazi tegemezi na kishazi huru.

 • Mtoto aliyevunjika mguu, amepelekwa hospitalini.                                        
 • Chombo kilichonunuliwa, kimetupwa jalalani.
 • Mle mlomokatazwa kuchunguzwa, mna mali nyingi.
 • Meli iliyofanyiwa marekebisho makubwa na serikali, imeanza safari zake. 
 • Alichagua, daftari lililojaradiwa jarada jekundu.

Ufunguo

Sehemu iloyoandikwa bila kukozwa= Kishazi huru

Sehemu iliyoandikwa kwa kukozwa = Kishazi tegemezi

Tungo Sentensi

Hii ni aina ya tungo ambayo imejengwa na kishazi kimoja au zaidi. Tungo hii ndiyo kubwa kuliko tungo zote na hutoa taarifa kamili. Sentensi huweza kuwa na neno moja au zaidi ilimradi tu itoe taarifa kamili. Pia, taarifa kamili hutolewa na kitenzi. Kwa hiyo hakuna sentensi iliyokamilika pasipo kitenzi.

Aina za Sentensi

Sentensi Sahili

Hii ni sentensi ambayo imejengwa na kishazi huru kimoja tu. Sentensi hii haina kishazi tegemezi kabisa. Tazama mifano hapo chini.

 • Mtoto anatemea kwa maringo.
 • Kijana shupavu anavuna miti.
 • Mwalimu anafundisha.

Sentensi Changamani

Hii ni sentensi ambayo imejengwa na kishazi huru kimoja na kishazi tegemezi kimoja au zaidi. Katika sentensi hii kuna urejeshi. Tazama mifano ifuatayo;

 • Tunda lililoiva, limeuzwa kwa bei nzuri.
 • Mgombea aliyepitishwa na tume, ameanza ya kufanya kampeni.
 • Kioo kilichovunjika, kimetupwa jalalani.
 • Redio iliyotangaza habari za uhuru, imefungwa.

Sentensi Ambatani

Hii ni sentensi inayojengwa na vishazi huru viwili. Pia, huweza kujengwa na vishazi huru viwili na kishazi tegemezi kimoja au zaidi. Kwa mfano;

 • Mama anapika na baba analima.
 • Mtoto aliyeugua malaria amepona na daktari aliyemtibu amemtembelea.
 • Ndoo imejazwa maji na sufuria ya ugali imeandaliwa.

Sentensi Shurutia

Hii ni sentensi inayojengwa na viambishi vya masharti. Masharti hayo ni kuwa jambo moja haliwezi kutendeka bila ya kutimiza jambo jingine linalokabiliana nalo. Tazama mifano ifuatayo:

 • Akija, nitampa.
 • Angalisoma, angalifaulu.
 • Angepewa dawa, angewahi kupona.
 • Angelihudhuria harusini, angalipewa zawadi nono.

Kutokana na mifano hapo juu tunaona kuwa sentensi shurutia hujengwa na viambishi vya masharti ambavyo ni kama vile;

 1. Ki na ta
 2. Nge
 3. Ngali na
 4. Ngeli

MUHIMU

Pamoja na kuwa sentensi shurutia hutajwa pahala pengi, lakini inazua mikinzano miongoni mwa wanazuoni. Hii ni kutokana kuwa inajikita zaidi katika umaana kuliko umuundo. Pamoja na hayo sentenzi hii inafanana kitabia na sentensi changamano. Kwa hiyo wanazuoni wengine hudai kuwa hauna sentensi shurutia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *