Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Mazingira ya Utunzi wa Kamusi

MAANA YA KAMUSI

Leech (1981:204) anasema, kamusi ni ghala la ukweli wote unaohusu lugha.

Kamusi ya Concise Oxford for Current English inasema, Kamusi ni kitabu kinachohusu neno mojamoja la lugha kwa ajili ya kuonesha tahajia, matamshi, maana na matumizi, usawe, vinyambuo na historia au kwa kiasi fulani baadhi ya ukweli unaofaa kama rejeo la maneno yaliyopangwa kwa namna inayoeleweka.

(Zugsta 1971:197) anamnukuu Beng kuwa kamusi ni mpangilio wa mfumo wa orodha ya maumbo yanayohusiana kiisimu yaliyokusanywa kutoka katika matamshi ya wazungumzaji na kupewa maoni ya mwandishi kwa namna ambayo msomaji mwenye sifa aweza kuelewa maana ya kila umbo na kuelekezwa taarifa zote zinazohusiana na matumizi ya umbo hilo katika jamii.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004) inasema kamusi ni kitabu cha maneno yaliyopangwa kwa utaratibu wa alfabeti na kutolewa maana na maelezo mengine.

Kwa ujumla tunaona kuwa kamusi ni kitabu kilichopo katika nakala ngumu au nakala tepe yenye orodha ya maneno ya lugha yaliyopewa maana na taarifa kuhusu matamshi, asili na matumizi au maneno ya lugha moja iliyopewa visawe vya lugha nyingine.

MAZINGIRA YALIYOPELEKEA UTUNZI WA KAMUSI

Mwanzo wa kamusi ni farahasa, matini za awali kabisa ambazo zinafikiriwa kuwa chimbuko la kamusi hazikuwa na umbo la kitabu wala maudhui kama tunavyoijua kamusi leo (Mdee 2010:10). Kihistoria inaonekana kuwa kamusi ilianza katika jamii zilizokuwa na ustaarabu wa kusoma na kuandika. Kamusi ya mwanzo kabisa ilitungwa katika nchi za mashariki ya kati (nchi za Kiakadi na Kisumeri) baadaye nchi kama China, India, Ugiriki, Roma pamoja na Iran ziliibua kamusi zao. Mazingira yaliyopelekea kuibuka kwa utunzi wa kamusi ni ugunduzi wa maandishi lakini mazingira mengine tunaweza kuyagawa katika makundi mawili ambayo ni mazingira ya kijamii na mazingira ya kiuchumi.

UGUNDUZI WA MAANDISHI

Kamusi huwekwa katika maandishi, hivyo jamii ambazo zilikuwa na elimu ya maandishi ndizo zilianza kuibua kamusi. Historia inaonesha kuwa jamii hizo zilianza kuwa na hitaji la ufafanuzi  wa misamiati mipya iliyotumiwa katika vitabu, magazeti na hata nyimbo. Mdee (2010:10) anasema Jamii isiyojua kusoma na kuandika hususani ile ambayo haikuingilina na watu wa jamii nyingine…… haikuhitaji kamusi

MAZINGIRA YA KIJAMII

Katika mazingira ya kijamii hasa haja zilizoibua utunzi wa kamusi ni kama zifuatazo;

  • Kutaka Kuelewa Tamaduni za Jamii Nyingine

Jamii ambayo ilivutiwa na tamaduni za jamii nyingine, ilipaswa kuandaa kamusi ili ipate kujifunza tamaduni hizo. Ili kujua tamaduni za jamii fulani lugha ya jamii ile huwa ndiyo nyenzo kuu. Katika kipindi cha miaka 4000 hadi 2000 KK Wasumeri walikuwa ni watu waliostaarabika sana hivyo Waakadi walitunga farahasa iliyowasaidia kupata tamaduni za kisumeri.

  • Kupata Elimu

Elimu hutolewa kwa lugha, elimu ya jamii moja huweza kuichochea jamii nyingine kutaka kupata elimu kama ile, basi ni lazima ijifunze lugha ya jamii yenye elimu ili iweze kupata elimu husika. Waakadi walipowatawala Wasumeri waliona kuwa pamoja na jamii ya Kiakadi kuwa na nguvu kilichokosekana ni elimu, kwa hivyo basi Waakadi walianza kujifunza lugha ya Kisumeri ili lugha hiyo iweze kupitisha elimu katika jamii yao. kutokana na hayo, msamiati wa Kisumeri uliorodheshwa na kupewa visawe katika Kiakadi.

Mdee (2010:11) anasema Waakadi walijifunza Kisumeri ili waweze kusoma katika taasisi za  Wasumeri zilizofundisha taaluma mbalimbali…. ili kuwasaidia wanafunzi….msamiati wa Kisumeri uliorodheshwa… pamoja na visawe vyake katika lugha ya Kiakadi.

  • Kujifunza Dini

Jamii ambazo zilitunza dini zao katika maandishi ziliweza kuandika farahasa yenye maneno yasiyojulikana na yanayopatikana kwenye dini hizo ili kuwarahisishia wajifunzaji. katika nchi ya India kulikuwa na kamusi za Sankriti ambazo zilitungwa kwa mtindo wa ushairi (Dash: makala). Katika jamii za Waingereza, farahasa za kiingereza zilikuwa na maneno magumu ya Kilatini yaliyonakiliwa kutoka katika vitabu vya kilatini (Mdee 2010:11). Farahasa za awali za kiingereza zilikuwa na maneno ya Kilatini…Kilatini kilikuwa lugha ya elimu ya dini huko Ulaya (Collison 1982).

  • Kutafsiri Maneno Yaliyoumika Katika Matini za Fasihi

Baada ya kuibuka fasihi andishi, fanani walitumia zaidi maneno yasiyojulikana, hivyo basi ili fasihi iweze kueleweka, kamusi zilitakiwa zitengenezwe. Nchini China kipindi cha Dynast (206 KK – 220 BK) sanaa ya utunzi wa kamusi ilikuwa ni sehemu ya kazi za fasihi pia ilikuwa ni kazi ya thamani katika kuelezea kazi za fasihi ya kale. Kamusi  zilizoibuka ni kama vile Yupian, Quiyun na Pahlaviki ambazo zilianzishwa kutokana na kukua kwa fasihi ya Persia ya sasa. Katika India kamusi iliyokuwapo ilijulikana kama NIGHUTU

  • Kujua Maana za Maneno Yasiyofahamika

Kamusi ziliweza kuibuliwa ili wanajamii waweze kujua maana ya maneno yasiyofahamika. Kutokana na maendeleo ya kujua kusoma na kuandika, wanajamii wengi walikuwa na hamu ya kusoma vitabu na matini mbalimbali, humo walikutana na maneno mapya, tatizo hili lilipatiwa ufumbuzi kwa kutumia kamusi. mifano ya kamusi hizi ni kama Amarakosa au Trikanda (sehemu tatu) ya India ilikuwa na taarifa zote ambazo wazungumzaji waliweza kurejelea, katika Kilatini kamusi kama  Shorte dictionarie na kamusi nyingine ni Shizhou kutoka China.

  • Kujua Maneno yenye Taarifa za Kijinsia

Haya ni mazingira mengine yaliyoibua utunzi wa kamusi katika jamii ya watu wa India. Kamusi iliweza kuibuliwa ili kukidhi haja ya ujuzi wa misamiati ya kijinsia. Kamusi ambazo zilibeba maudhui hayo ni kama vile; Ligadi na Sangraha ambazo ziliitwa kwa pamoja kama kamusi ya LINGA.

  • Hiaji la Kuwasiliana na Watu wa Mataifa Mengine

Jamii moja ilipohitaji kuwasiliana na jamii nyingine ilipaswa kujua lugha itumiwayo na jamii hiyo, hivyo basi kamusi ilikuwa ni kiungo muhimu kwa jamii hizo. Mfano wa kamusi hizo ni A Worlde of Words Italian – English, Lesclarcissement de Langue Francoys (Kiingereza Kifaransa).

Mdee (2010:14) kamusi ya John Palsgrave (1530) ilikusudiwa iwasaidie waingereza  wajifunze kifaransa ili waweze kuishi Ufaransa bila matatizo.

MAZINGIRA YA KISIASA

Wakoloni walitunga kamusi ili ziweze kuwasaidia katika utawala wao. Katika Afrika Mashariki wakoloni walitunga kamusi ili waweze kujifunza Kiswahili na kisha  kuwafundisha wa kwao ili wakija Afrika Mashariki wawe na angalau ujuzi wa Kiswahili. Kamusi ambazo zilitungwa ni kama vile A Standard English Kiswahili Dictionary, English Sowel, English Sid, English Sowhel, na English Sowahel.

MAJUMUISHO

Kwa ujumla tumeona kuwa maendeleo ya maandishi yamechangia kwa kiasi kikukubwa sana kuibuka kwa kamusi. Maarifa ya jamii moja huweza kupitishwa kwa jamii nyingine endapo jamii ya awali itajifunza lugha ya jamii husika. Hivyo suluhisho ni utunzi wa kamusi ambao huwa na maneno yaliyo katika lugha moja na ya lugha nyingine, lakini pia kamusi wahidiya ilitumiwa na wazawa ili waweze kung’amua maneno yasiyojulika katika lugha yao.

MAREJELEO

Collison, R.L. (1982) A History of Foreign Language Dictionaries, Andre Deutch. London

Dash, The Art of Lexicograph  (makala)

Lipka, L. (1992) A outline of English Lexicography, Tubingen. Germany.

Massamba na wenzake, (2009) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu, TUKI. Dar es salaam

Mbaabu, I. (2007) Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili, TUKU. Dar es salaam

Mdee, J.S  J.S (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia, TUKI. Dar es salaam

Shiqi, X. (1982) Chines Lexcography, Myson. India

Zgusta, L. et al. (1971) Manual of Lexicography, The Hague. India.

8 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *