Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

ISIMU, ISIMUJAMII NA SOSIOLOJIA YA LUGHA

Utangulizi

Kazi hii imekusudia kufafanua kwa ufasaha tofauti za msingi kati ya isimujamii na sosiolojia ya lugha pamoja na kuelea jinsi isimu na isimujamii zinavyokamilishana katika malengo yake. Hivyo, kazi hii itakuwa na sehemu nne, ambapo sehemu ya kwanza itaeleza maana ya isimu, maana ya sosiolojia ya lugha na kisha maana ya isimujamii. Kisha sehemu ya pili itaelezea kuhusu tofauti kati ya isimujamii na sosiolojia ya lugha. Sehemu ya tatu itahusu malengo ya isimu na isimujamii na kuelezea namna taaluma hizo zinavyokamilishana kimalengo. Ndipo sehemu ya nne ni hitimisho litalohusu majumuisho.

Maana ya Isimu

isimu ni sayansi ya lugha (Crystal, 2008:283). Mekacha (2011:11) anasema, Isimu ni taaluma inayojishughulisha na utafiti, ufafanuzi na uchambuzi wa lugha. Taaluma hii huzingatia vipengele vya lugha ambavyo ni fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki ambapo kila kipengele kina kazi yake mahsusi.

Kwa hiyo kulingana na wataalamu hao, tunaona kuwa isimu ni taaluma ya lugha inayoshughulika na utafiti, ufafanuzi na uchambuzi wa lugha. Taaluma hii hushughulikia sauti, maumbo, miundo na maana za maneno katika lugha kwa jumla ama lugha mahsusi.

Maana ya Isimujamii

Isimujamii ni taaluma inayotafiti, kuchanganua na kufafanua uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii (Holmes 1992, Romaine 1994)[1]. King’ei (2010:11) anafasili isimujamii kuwa ni taaluma inayoeleza uhusiano wa karibu uliopo kati ya matumizi ya lugha na masuala ya jamii.

Kwa ujumla isimujamii hushughulikia uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii. Katika taaluma hii jamii na lugha hukamilishana. Kwa hiyo bila kuwepo kwa jamii hakuna lugha. Pia lugha ni kitu muhimu katika jamii kwani huweza kutambulisha jamii.

Maana ya Sosiolojia ya Lugha

Hii ni taaluma inayohusika na uchambuzi na ufafanuzi  wa muundo wa jamii hususani kama inavyojidhihirisha kutokana na tofauti katika matumizi ya lugha (Mekacha 2014:41). Sosiolojia ya lugha huhusika na namna lugha inayotumika hasa katika jamii lugha uwili ama ulumbi, pia huangalia sera ya lugha katika jamii.

Tofauti kati ya Isimujamii na Sosiolojia ya Lugha

Katika kuangalia tafauti baina ya isimujamii na sosiolojia ya lugha wataalamu kama Fishman,Trudgil na Fasold, wanaona kuwa tofauti ipo katika nadharia ya lugha kama nyenzo. Pia wanaona kuwa jamii ni pana zaidi kuliko lugha na ndiyo inayotoa muktadha wa lugha kufanya kazi. Lugha ipo kwa ajili ya jamii na jamii ndiyo inayofanya lugha kuwa kama ilivyo (Mekacha 2000:27). Kwa hiyo tofauti baina ya isimujamii na sosiolojia ya lugha ni kama zifuatazo;

Isimujamii na sosiolojia ya lugha hutofautiana katika malengo. Lengo la isimujamii ni kuchunguza, kuchambua na kufafanua tofauti zilizomo katika lugha, wakati lengo la sosiolojia ya lugha ni kuchambua na kufafanua muundo wa jamii hususani kama unavyojidhihirisha katika matumizi ya lugha.

Tofauti nyingine ni kuwa isimujamii ni mojawapo ya taaluma kati ya taaluma za isimu, ambapo kila kipengele ambacho ni cha kiisimujamii lazima kiwe na isimu ndani yake wakati sosiolojia ya lugha ni miongoni mwa taaluma za sosiolojia yaani hushughulika na masuala ya jamii na utamaduni wake (Mekacha 2000:28).

Isimujamii inamhusu mwanalugha ambaye huanza kufanya uchunguzi kwa kufasili lugha na vipengele vyake kisha kuchunguza jinsi matumizi ya lugha yanavyoathiriwa na jamii, wakati sosiolojia ya lugha inahusu mtaalamu wa masuala ya jamii ambaye huanza uchunguzi wake kwa kufasili jamii na misingi yake kisha kuchunguza namna misingi hiyo ya jamii inavyowiana na matumizi ya lugha.

Pia isimujamii hushughulikia tofauti za lugha huku ikitilia mkazo lugha na vipengele vyake kama matamshi, maumbo ya maneno, miundo ya sentensi na maana wakati sosiolojia ya lugha hushughulikia tofauti zilizopo kati ya jamii kwa kuzingatia matabaka na makundi ya watu katika jamii kulingana na hadhi, kazi na jiografia.

Tofauti nyingine ni kuwa isimujamii huweka msisitizo katika ufafanuzi wa lugha kadri unavyohusiana na jamii wakati sosiolojia ya lugha huweka msisitizo kwa jamii kadri inavyohusiana na lugha.

Pia msingi wa isimujamii umejengwa katika kuijua lugha kwanza kisha kuihusianisha na jamii wakati msingi wa sosiolojia ya lugha umejengwa katika kuijua jamii kwanza kisha kuihusianisha na lugha.

Kwa ujumla tunaona kuwa isimujamii na sosiolojia ya lugha ni taaluma ambazo kimsingi zina dhima moja, ambayo ni kuchunguza jamii na kuchunguza lugha (isimu). Ingawa isimujamii huanza kwa kuifasili lugha na sosiolojia ya lugha huanza kwa kuifasili jamii lakini hitimisho huwa moja.

Malengo ya Isimujamii

Lengo la isimujamii ni kuchunguza tofauti za utumiaji wa lugha katika jamii na kuzitolea ufafanuzi tofauti hizo. Mwanaisimujamii huchunguza namna mzungumzaji anavyochagua lugha ya kutumia kama ni rasmi ama si rasmi, pia namna mzungumzaji anavyoteua maneno kulingana na uhusiano alionao na msikilizaji (Msanjila na wenzake 2011:6). Kwa mfano, mfanyakazi anapozungumza na mfanyakazi mwenzake ni tofauti na jinsi anavyozungumza na mkuu wake wa kazi.

Lengo la pili ni kuchunguza na kufafanua uhusiano uliopo baina ya lugha na azungumzaji. Hapa mwanaisimujamii huchunguza namna mwanajamii anavyojibainisha kwa kutumia lugha. Kwa kutumia vibainishi vya isimu lengo hili huonesha imani ya mzungumzaji, eneo atokalo, jinsia yake ama kiwango chake cha elimu (Msanjila na wenzake 2011:8).

Pia isimujamii huchunguza na kufafanua uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine katika jamii. Katika lengo hili mwanaisimujamii huchunguza namna lugha zinavyohusiana katika jamii. Pia huchunguza dhima za lugha hizo katika jamii hiyo, kama ni lugha ya taifa, lugha rasmi ama lugha ya wazungumzaji wachache.

Isimujamii pia huchunguza mandhari lugha, ambapo wanaisimujamii huchunguza namna lugha zinavyotumika katika matangazo ya biashara katika lununga, redio na mabango. Lugha hizo maranyingi ni tofauti na lugha zinazotumiwa katika mazungumzo ya kawaida.

Malengo ya Isimu

Lengo la isimu ni kuchunguza na kuchambua taratibu zote zinazohusiana na utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla (Massamba na wenzie, 2013:5). Hapa mwanaisimu huangalia namna mtoaji wa sauti jinsi anavyotoa na namna msikilizaji anavyosikia na kuifasili sauti hiyo.

Lengo lingine ni kuchambua, kuainisha na kuchunguza sauti pambanuzi za lugha za binadamu. Sauti zinazotumika katika kutofautisha maana za maneno katika lugha (Massamba na wenzie 2013:6). Kila lugha ina sauti zake mahsusi. Hivyo, mwanaisimu huchunguza mahali pa kutamkia na tabia za sauti za lugha mahsusi pia huangalia mpangilio wa silabi za lugha hiyo.

Pia isimu huchunguza jinsi maneno ya lugha asilia yanavyoundwa (Chomi 2013). Katika sehemu hii mwanaisimu huchunguza namna viambishi mbalimbali vinavyojenga maneno.

Vivyo hivyo, isimu huchunguza mpangilio wa maneno. Katika sentensi kuna mpangilio mahsusi wa maneno. Hivyo mwanaisimu anachochunguza ni namna gani maneno hupangiliwa katika lugha ili kujenga sentensi yenye maana. 

Lengo lingine ni kuchunguza maana za maneno na sentensi. Dhumuni kubwa la lugha ni kuwasiliana, ili kukamilisha dhumuni la mwanaisimu huangalia maana zinavyojitokeza katika maneno na sentensi. Maana hizo ndizo kiini cha mawasiliano.

Pia isimu huchunguza namna lugha zinavyotumika katika muktadha tofauti tofauti. Kwa mfano, namna lugha inavyotumika sokoni ni tofauti na lugha inavyotumika shuleni.

Isimu na Isimujamii Zinavyokamilishana Kimalengo

Isimu na isimujamii zote ni taaluma zinazoshughulikia lugha asilia[2]. Katika isimu lugha hushughulikiwa katika vipengele vya kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki. Isimujamii hutafiti na kufafanua tofauti zilizomo ndani ya lugha (isimu) na namna zinavyohusiana  na tofauti zilizopo katika jamii (Mekacha, 2000:18).

Isimu na isimujamii hukamilishana kimalengo, kwani kimantiki isimujamii ni taaluma inayohusisha taaluma ya isimu na taaluma ya jamii. Hivyo ili kuifikia lengo la isimujamii ni lazima mwanaisimujamii aichunguze taaluma ya isimu. Kwa mfano, ili kujua matabaka ya wanajamii, mwanaisimujamii hana budi kuchunguza namna lugha (isimu) inavyotumiwa na wanajamii hao.

Pia lengo la isimujamii ni kuchunguza lugha inavyotumiwa katika jamii. Hivyo mwanaisimujamii hana budi kuifahamu taaluma ya isimu na vipengele vyake. Kwa kutumia vipengele vya kiisimu, mwanaisimujamii huweza kuchunguza uhusiano wa lugha na wazungumzaji ili kutambua imani za wazungumzaji hao, jinsia ama maeneo yao.

Malengo ya isimu na isimujamii yanakamilishana kwani yote huangalia matumizi ya lugha katika mazingira lugha hiyo itumikayo. Isimu huangalia tofauti za lugha katika mazingira tofauti. Kwa mfano, mahakamani, katika biashara na hata katika nyumba za ibada. Pia isimujamii katika lengo la mandhari lugha huangalia namna lugha inavyotumika katika matangazo.

Kwa ujumla taaluma ya isimu na isimujamii hukamilishana, kwani taaluma ya isimujamii hushughulikia pia taaluma ya isimu. Mwanaisimujamii huanza kuichunguza lugha kisha kuangalia namna jamii inavyoiathiri lugha hiyo. 

Marejeleo

Chomi, W. E (2013), Kitangulizi cha Mofolojia, Dar es Salaam: TUKI

King’ei, K. (2010), Misingi ya Isimujamii, Dar es Salaam: TUKI

Massamba na wenzie. (2013), Fonolojia ya Kiswahili Sanifu, Dar es salaam:    

           TUKI

Mekacha R DK (2000), Isimujamii:Nadharia na Muktadha wa Kiswahili, Osaka   

           University:

Mekacha, R. D. K (2011), Isimujamii: Nadharia na Muktadha wa Kiswahili,

           Dar es Salaam: TUKI

Msanjila, Y. P. na wenzie (2011), Isimujamii Sekondari na Vyuo, Dar es

           Salaam: TUKI.


[1] Kama walivyonukuliwa na Mekacha (2011:23)

[2] Lugha asilia ni lugha zinazotumiwa na binadamu (Massamba na wenzake 2013:1)

390 Comments