Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

AINA ZA MAANA

Karibu katika makala haya ambayo tunajadili kuhusu maana ya maana pamoja na aina zake.

MAANA YA MAANA (Maana ni nini?)

Maana ya maana ni dhana iliyoshughulikiwa kwa mtazamo tofauti na wanazuoni tofauti. Habwe na Karanja (2007: 205) wanasema “dhana ya maana ni ya kidhahania kwa sababu haina muundo thabiti…. Maana kwa hiyo ni dhana tata ambayo si rahisi kueleweka kwa uwazi”

Kamusi ya Oxford Advanced Learner’s (2010:920) imefasili maana ya maana kuwa ni kitu au wazo ambalo ishara, neno ama sauti huwakilisha.

Ullman (1977:54) anamnukuu Profesa Firth kuwa ili kuweza kuwa na maana ni lazima kuwe na uhusiano wa kimazingira kati ya fonetiki, leksikografia na matumizi sahihi ya maneno.

Leech (1981:2) anawaonesha wanazuoni Ogden na Richards kuwa wao waliorodhesha maana za maana takribani ishirini, ikiwemo inayodai maana ni ile ambayo mtumiaji wa ishara anapaswa kuirejerea.

Kwa ujumla tunaona kuwa maana ni tata kwani wanazuoni wengi hawakubaliani ni maelezo yapi yanaweza kubeba maana ya maana.

Pamoja na hayo tunaweza kusema kuwa, maana ni alama, ishara, dhana, maneno au neno linalotumika kueleza kuhusu kitu, mtu au jambo fulani.

AINA ZA MAANA

Uainishaji wa maana upo katika mitazamo tofauti ya wanaisimu. Hata hivyo, hatuna budi kuzichambua aina mbalimbali za maana kama zilivyoelekezwa na wataalamu mbalimbali kulingana na mitazamo yao. Leech (1981:8 – 9) anaainisha maana katika aina saba kama ifuatavyo;

MAANA YA MSINGI (Conceptual meaning)

Maana hii ni kiini cha nawasiliano katika lugha. Aina hii ya mawasiliano hubeba sifa za kisintaksia na kimofolojia. Hii ni maana ambayo haibadiliki kulingana na mazingira, pia huwa na sifa bainifu na sifa ya kimuundo. Neno huweza huweza kupata maana baada ya kuwekewa sifa bainifu kwa mfano;

Mti       + kiumbe hai

              – mnyama

             + mizizi

Lakini katika upande wa kimuundo maana huweza kupatikana baada ya viambajengo kuungana na kuunda kiambajengo kimoja kikubwa chenye maana. Kwa mfano; N + V + T + E = S

MAANA KIDHAMIRA (Thematic meaning)

Maana hii hupatikana baada ya muongeaji ama mwandishi kupanga ujumbe wake kwa msisitizo, mpangilio na umakini. Hapa maana hubebwa na kitu kinachodhamiriwa, kwa mfano;

 1. Chungwa limeliwa na Juma
 2. Juma amekula chungwa

Katika sentensi ya kwanza dhamira ya kutaka kujua ipo kwenye chungwa. Swali linaweza kuwa chungwa lipo wapi? Lakini katika sentensi ya pili dhamira ipo kwa Juma. Swali linaweza kuwa Juma amekula nini?

MAANA HUSIANISHI (Connotative meaning)

Hii ni maana ambayo hupatikana baada ya kuhusisha historia, sheria na utamaduni wa jamii fulani. Maana huweza kukipa sifa kitu kulingana na maana ya jamii husika, mfano mwanamke anaweza akapewa sifa ya upole, uoga, ama ulinzi, hivyo mwanaume anaweza akaitwa mwanamke kwa sababu ana moja ya sifa ya mwanamke pia mara nyingi mtu mzima asipojiheshimu watu humwambia “ACHA UTOTO”

Pamoja na hayo maana msingi hutofautina toka jamii moja na nyingine.

MAANA YA KIJAMII (Social meaning)

Hii ni maana ambayo tunaipata kutokana na tofauti za kitamshi na matumizi ya maneno au misamiati. Kwa kimsikiliza mtu na jinsi anavyochagua misamiati yake na mtindo wake wa mawasiliano tunapata kujua hadhi yake huyo mtu, kwa mfano;

 1. Waliwagonga mandata kisha wakasepa na mawe yote.
 2. Waliwapiga polisi kisha wakakimbia na pesa zote.

Hivyo mtu huchagua ni yupi kati ya aliyezungumza sentensi ya kwanza au ya pili anatoa taarifa iliyosahihi. Hata hivyo hizo sentensi zinatuonesha ni tabaka lipi lipo katika sentensi ipi.

MAANA REJEREZI (Reflected meaning)

Hii ni maana ambayo maana moja ya msingi hurejerea maana ya msingi nyingine. Hii inamaanisha maana ya msingi hupewa sifa ya maana nyingine ya msingi, kwa mfano; ua = msichana, pia maana rejerezi huweza kutumika kama tasfida, mfano; uani = chooni.

MAANA TANGAMANI (Collocative meaning)

Hii ni maana ambayo huhusisha neno moja na neno lingine kulingana na mazingira yake. Mfano; neno mtanashati huhusisha jinsia ya kiume wakati mrembo huhusisha jinsia ya kike, pia neno kama wifi, shangazi, mjoba hata baba huhusisha jinsia.

Pamoja na Leech, wataalamu wengine ni Habwe na Karanja (2007:204 – 206) wanaogawa maana katika aina kuu mbili, kwanza kuna maana ya kileksika na maana kisarufi.

MAANA YA KILEKSIKA

Hii ni maana ambayo wanasema ni maana iliyopo katika kiwango huru cha neno. Maana hii ni ya kikamusi ambayo pia huitwa maana ya msingi, maana hii huwa haibadiliki kulingana na athari za kimazingira.

MAANA YA KISARUFI

Aina hii ya maana hurejerea maana katika muktadha wa matumizi. Hivyo hii pia tunaweza kuita maana ya ziada. Maana ya ziada huweza kuwa na aina zingine za maana ambazo ni;

 1. Maana Husishi ambayo huhusisha neno na hali fulani, mfano neno mfalme huhusishwa na fahari lakini njaa huhusishwa na umasikini.
 2. Maana Elezi, hii hupatikana baada ya kuonesha kitu kwa kunyooshea kidole.
 3. Maana ya Umaanisho, hii ni maana ambayo mtu husema kitu kimoja na kumaanisha kingine. Hii ni maana ya msemaji. Mfano,

          Mama: Naona nyote mmeshalala.

          Watoto: (wanaenda kulala) baada ya kusikia maneno ya mama yao.

Mtaalamu mwingine ni Matinde (2012), anayeainisha maana katika aina kuu tatu kama ifuatavyo;

MAANA TAMBUZI

Hii ni maana ya msingi ambayo imeundwa katika msingi wa kileksika. Maana hii inarejerea katika kamusi kama ilivyoelezwa na kukubaliwa na wataalam wengine.

MAANA HUSISHI

Hii maana hutokana na uhusishaji wa maana ya neno moja katika kudokeza maana ya neno lingine. Mafinde aliigawa maana hii katika sehemu nne kama ifuatavyo;

 1. Maana Ashirifu, hii ni maana inayotokana na hisia na matakwa ya msemaji, kwa mfano, Ali ni simba. Simba ikiashiria mtu mkali.
 2. Maana Shawishi, hii huongezewa vijenzi mbalimbali ili kueleza hisia za msemaji, maranyingi hujitokeza kwenye mahubiri ya kidini, hotuba za kisiasa na pia kwenye biashara, kwa mfano kwenye biashara maneno kama sabuni takasa, redio bomba, ukweli na uhakika, yote hulenga kumshawishi mteja.
 3. Maana Kijamii, hii hukitwa katika jamii, maana za maneno huweza kutofautiana kutoka jamii moja na nyingine, mfano sentensi, maji ya bomba, hutumia zaidi Tanzania bara wakati visiwani husema maji ya mferejini.
 4. Maana Endanifu, hii ni maana inayotokana na uhusiano wa kimantiki kati ya maneno ambayo yametumiwa katika sentensi au tamko, mfano mtanashati huendana na mvulana wakati mrembo huendana na msichana.

MAANA DHAMIRIFU

Hii ni maana ambayo hutegemea kile msemaji amedhamiria kukisisitiza katika usemi wake kwa kuzingatia mazingira mahsusi ya kiisimu, mfano;

 • Maziwa yamemwangwa na mtoto
 • Mtoto amemwaga maziwa

Katika sentensi ya kwanza msisitizo uko kwenye maziwa wakati katika sentensi ya pili uko kwa mtoto.

Kutokana na wataalamu hao ambao kwa kiasi kikubwa wamekubaliana aina za maana ingawa utofauti uko katika misamiati pamoja na mgawanyo wa aina za maana, tunaona kuwa aina za maana zipo tatu, ambazo ni;

MAANA YA MSINGI, ambayo ndio maana isiyobadilika kulingana na athari za kimazingira, pia ni maana ya kikamusi. Maana hii ndiyo huzaa aina zingine za maana, hivyo basi maana ya msingi ndiyo maana kuu, hata hivyo haimaanishi kuwa aina zingine za maana hupaswa kupuuzwa, maana ya msingi hutegemea pia aina zingine za maana ili ujumbe uliokusudiwa uweze kufikishwa kwa namna tofauti.

MAANA YA KIDHAMIRA, maana hii huonesha zaidi kusudio la mwandishi ama msemaji, pale palipowekwa msisitizo ndipo panapobeba maana, maana hupatikana palipowekwa vipamba lugha.

MAANA HUSISHI, hii ni maana ambayo hutokana na maana ya msingi, maana hupatikana hasa ambapo mazingira yameathiri maana ya msingi hivyo tunapata, maana iliyoathiriwa na jamii, hisia, urejezi na utangamano.

HITIMISHO

Wataalamu wengi wa isimu wameweza kuzigawa aina za maana katika makundi tofauti, ingawa bado hakuna uwiano mkubwa sana lakini wote wanakubaliana kuwa maana ya msingi ndiyo kitovu cha maana, hivyo huzaa maana zingine pia wanaona kuwa maana ya msingi haiathiriwi na mazingira lakini ukweli ni kwamba maana ya msingi inapokutana na mazingira ya usinonimia na mahusiano mengine ya maneno huweza kuathiriwa, kwa mfano maneno kama shule na skuli, bomba na mfereji, sembe na sima, hoho, leso na kanga pamoja na uzi na kamba, huwa na maana moja ambapo matumizi hutegemea mazingira husika.

MAREJEREO

Habwe, J na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Phoenix publisher LTD, Nairobi.

Leech, G. (1981) Semantics the Study of Meaning, Penguin Books, England.

Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, Serengeti Education publisher(T)

                LTD, Mwanza.

 Mwihaki, A. Meaning as Use, A Functional View of Semantics and Pragmatics. (matini)

Ullman, S. (1977) Semantics an Introduction to the Meaning, Basil Blackwell and Mott LTD,

                        London.

28 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *