Tuesday, October 20Kiswahili kitukuzwe!

NGELI ZA NOMINO

Karibu tena katika mwendelezo wa makala haya yanayojikita katika kutoa maarifa ya Kiswahili kwa kidato cha tatu. Leo tutajadili kuhusu ngeli za nomino na viambishi vyake vya urejeshi.

Ngeli humaanisha kundi au aina.

Ngeli za Nomino ni nomino zenye tabia sawa zinazowekwa katika kundi moja. Makundi hayo huwekwa kwa huzingatia vigezo mbalimbali. Vigezo hivyo ni kama vile; kigezo cha kimofolojia na kisintaksia au cha upatanisho wa kisarufi. Hata hivyo, kigezo kitachotumika hapa ni cha  kisintaksia.  

Kigezo cha kisintaksia kinaangalia viambishi awali vya kitenzi vijengavyo ngeli. Kwahiyo kundi la nomino linategemea kitenzi.

S/NNGELIMifano (Umoja)Mifano (Wingi)Urejeshi
1A – WAKijana anakuja.Vijana wanakuja.ye – o
2U – IMti umekatika.Miti imekatika.o – yo
3LI – YAChungwa limeoza.Machungwa yameoza.lo – yo
4KI – VIKiatu kimeisha.Viatu vimeisha.cho – vyo
5I – ZITiketi imepatikana.Tiketi zimepatikana.yo – zo
6U – ZIUzi umekatika.Nyuzi zimekatika.o – zo
7U – YAUasi umeongezeka.Maasi yameongezeka.o – yo
8KU-Kucheza kunafurahisha ko
9PA MU KUPale panatisha
Mule mnatisha
Kule kunatisha
 po
mo
ko

Kigezo hiki huzingatia upatanishi wa kisarufi katika sentensi. Kwa hiyo, ili kung’amua nomino ipo katika kundi lipi, inapaswa kutunga sentensi ya umoja na wingi kasoro katika ngeli ya nane na ya tisa. Nomino za ngeli ya nane na ya tisa hazina umbo la umoja wala la wingi.

Pia, viambishi vinavyoonesha ngeli ni vile viambishi awali vya kitenzi vinavyoonesha umoja na wingi. Tutazame sifa za nomino kwa kila ngeli.

a – wa

Ngeli hii hujumuisha majina ya wanyama wote. Kama vile; watu, wadudu, ndege, samaki, n.k. Kwa mfano;

UmojaWingi
Mtoto analima.Watoto wanalima.
Kipofu amepewa zawadi.Vipofu wamepewa zawadi.
Mwalimu anafundisha.Walimu wanafundisha.
Kichaa amekula chungwa chafu.Vichaa wamekula machungwa machafu.
Siafu amebeba nyasi.Siafu wamebeba nyasi.
Kupe anaishi siku nyingi bila kula.Kupe wanaishi siku nyingi bila kula.

u – ya

Nomino ambazo zinakiambishi awali {u} katika umoja na {ma} katika wingi huangukia katika kundi hili. Kwa mfano;

UmojaWingi
Unyoya umepeperuka.Manyoya yamepeperuka.
Uuaji umedhibitiwa.Mauaji yamedhibitiwa.
Uasi umekithiri.Maasi yamekithiri.
Ugonjwa umepungua.Magonjwa yamepungua.
Ugumu umempata.Magumu yamempata.

 u – zi

Katika ngeli hii yanaingia majina yenye viambishi awali kapa {Ø} au {w} katika umoja na vinavyoanzia na {ny-} na baadhi huwa na kapa katika wingi. Kwa mfano;

UmojaWingi
Uzi umekatika.Nyuzi zimekatika.
Ungo umechafuka.Nyungo zimechafuka.
Ufa umeongezeka.Nyufa zimeongezeka.
Wembe umemkata.Nyembe zimemkata.
Uso umepauka.Nyuso zimepauka.
Ubao umechanwa.Mbao zimechanwa.

u – i

Hii ni ngeli ambayo nomino zinazoingia ni zile zinazoanzia na kiambishi {m-} katika umoja na {mi-} katika wingi. Kwa mfano;

UmojaWingi
Mti umepandwa.Miti imepandwa.
Mpera umeanguka.Mipera imeanguka.
Msitu umehifadhiwa.Misitu imehifadhiwa.
Mlango umepakwa rangi.Milango imepakwa rangi.
Mguu umeimarika.Miguu imeimarika.

li – ya

Katika kundi hili nomino zenye kiambishi kapa katika umoja na kiambishi {ma} katika wingi huhusishwa. Kwa mfano;

UmojaWingi
Gari limetengenezwa.Magari yametengenezwa.
Tairi limeshonwa.Matairi yameshonwa.
Jambo limefafanuliwa.Mambo yamefafanuliwa.
Jino linauma.Meno yanauma.
Kopo limeyeyushwa.Makopo yameyeyushwa.
Ini linachuja sumu.Maini yanachuja sumu.

i – zi

Ngeli hii hujumuisha majina mengi ambayo hayabadiliki umbo katika umoja na wingi wake. Kwa mfano;

UmojaWingi
Salamu imenifikia.Salamu zimenifikia.
Kazi imenibana.Kazi zimenibana.
Nguzo imesimikwa.Nguzo zimesimikwa.
Kalamu ina ufutio.Kalamu zinaufutio.
Simu itamaliza chaji.Simu zitamaliza chaji.

ki – vi

Mara nyingi hujumuisha majina ya vitu visivyo hai yanayoanzia na kiambishi {ki-} katika umoja na {vi-} katika wingi. Kwa mfano;

UmojaWingi
Kiti kimevunjika.Viti vimevunjika.
Kiazi kimeiva.Viazi vimeiva.
Kiatu kimeshonwa.Viatu vimeshonwa
Kichwa kinauma.Vichwa vinauma
Kitambaa kimenunuliwaVitambaa vimenunuliwa

ku

Nomino zote zinazotokana na vitenzi huingizwa. Majina hayo hutokana na kuambika kiambishi awali {ku} katika katika kitenzi. Kwa mfano;

  • kucheza kunafurahisha.
  • Kula kunaleta afya.
  • Kufua kunawakilisha usafi.

PAMUKU

Ngeli hii inajalizwa na majina yanayoonesha mahali. Kwa mfano;

  • Pale panatisha.
  • Mule mnatisha.
  • Kule kunatisha.

Pale hutumika kuonesha mahali mahususi. Mulehutumika kuonesha mahali pa ndani na kule hutumika kuonesha mahali pa jumla.

UREJESHI KATIKA NGELI

Viambishi vya ngeli huweza kushikamana na viambishi vya urejeshi. Tazama jedwali lifuatalo kwa mifano;

S/NNGELIUrejeshiMifano (Umoja)Mifano (Wingi)
1A – WAye – oMtoto aliyeokota janiWatoto waliookota jani
2U – Io – yoMti uliopandwaMiti iliyopandwa
3LI – YAlo – yoGari lililoharibikaMagari yaliyoharibika
4KI – VIcho – vyoKiatu kilichonunuliwaViatu vilivyonunuliwa
5I – ZIyo – zoSalamu iliyomfikiaSalamu zilizomfikia
6U – ZIo – zoUngo uliochafukaNyungo zilizochafuka
7U – YAo – yoUnyoya uliopeperukaManyoya yaliyopeperuka
8KU-koKucheza kunakofurahisha 
9PA MU KUpo mo koPale panapoonekana Mule mnamoonekana Kule kunapoonekana

Asante kwa kuwa pamoja nasi na karibu tena kwenye makala yafuatayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *