Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

MAUDHUI

Karibu tena kwenye makala zetu zilizojikita kutoa maarifa ya Kiswahili kwa kidato cha tatu. Leo tutajadili kuhusu maudhui na vipengele vyake.

Maudhui ni nini?

Maudhui ni jumla ya mawazo yote ya mwandishi katika kazi ya fasihi. Maudhui hujumuisha vipengele vifuatavyo;

  1. dhamira
  2. ujumbe
  3. migogoro.
  4. falsafa na
  5. mtazamo

Dhamira

Ni lengo au kusudio la msanii analotaka liifikie hadhira yake. Kuna aina mbili za dhamira ambazo ni; dhamira kuu na dhamira ndogondogo.

Dhamira Kuu

Ni dhamira ambayo hubeba wazo kuu la mwandishi.

Dhamira ndogondogo

Ni dhamira ambazo hubeba mawazo mengineyo yajengayo dhamira kuu.

Ujumbe/Maadili/Mafunzo

Hili ni funzo ambalo hadhira hulipata awasilishiwapo kazi ya fasihi. Funzo hili hutokana na dhamira zilizopo katika kazi yenyewe. Kwa hiyo dhamira ndizo huzaa ujumbe.

Falsafa/Msimamo

Hii ni imani ya mwandishi kuhusu maisha kwa ujumla. Msanii anaona maisha hujengwa na jambo gani hasa? kuna nini katika mazingira ya mwanajamii? n.k.

Imani hii hujengeka kulingana na tajiriba aliyoipata msanii. Hata hivyo ili kujua imani ya mwandishi kuhusu maisha yatupasa kusoma kazi zake nyingi.

Mtazamo

Hii ni namna msanii anavyoyaona mambo mbalimbali ya kimaisha. Kuhusu matatizo yaikumbayo jamii na namna bora ya kuyasuluhisha.

Kutokana na hilo, tunakupata aina mbili za mitazamo. Aina hizo ni; mtazamo wa kiyakinifu na mtazamo wa kidhanifu.

Mtazamo wa Kiyakinifu

Huu ni mtazamo ambao msanii huonesha matatizo yanayoikumba jamii kisha hutoa suluhisho linaloweza kupimika. Yaani suluhisho dhahiri. Kwa mfano, ili kuondoa umasikini yatupasa kufanya kazi kwa bidii.

Mtazamo wa Kidhanifu

Huu ni mtazamo ambao msanii huonesha matatizo yanayoikumba jamii kisha kutoa suluhu ambalo haliweza kupimika yaani siyo halisia. Kwa mfano, ili kuondoa matatizo ya kijamii yatupasa kusali sana au kumuachia Mungu.

Migogoro

Hii ni mivutano au hali ya kutokukubaliana kuhusu mambo mbalimbali kati ya pande mbili. Yaweza kutokea kwa mhusika mmoja na mwingine, mhusika na kikundi au jamii, wahusika na wahusika wengine, jamii na jamii, tabaka na tabaka au mhusika na nafsi yake mwenyewe.

Kuna aina mbalimbali za mogogoro kama ifuatavyo;

  • Migogoro ya kisiasa

Hii hutokea kutokana kutokana na migongano ya kiitikadi baina ya pande mbili.

  • Migogoro ya kiuchumi

Hii hutokea aina ya wenye nacho na wasio nacho. Wenye nacho hujitahidi kumkandamiza asiye nacho ilhali asiye nacho hupambana ili kujikwamua na umasikini.

  • Migogoro ya kiutamaduni

Hii hutokea hasa baina ya ukale na usasa. Wengine huamini tamaduni za kale wakati wangine wanadai mabadiliko ya kiutamaduni.

  • Mgogoro wa nafsi

Hii ni mikinzano inayotokea katika nafsi ya mhusika pale anapokuwa njia panda. Yaani hajui achague kufanya jambo gani kati ya anayoyaona au yanayomtatiza.

Kwa ujumla fani na maudhui ni vipengele vyenye uhusiano wa kimjengano. Kwa hiyo, hatuwezi kuwa na maudhui pasina fani na kinyume chake ni sahihi.

Tafadhali endelea kufuatilia makala zetu kwa maarifa zaidi.

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *