Karibu tena kwenye mwendelezo wa makala zetu zilizojikita katika nukuu za Kiswahili kidato cha tatu. Leo tutajadili kuhusu Fani na vipengele vyake.

Fani ni nini?
Fani ni nui au ufundi anaoutumia msanii wa fasihi katika kuwasilisha mawazo yake. Tunaweza kusema pia, fani ni namna msanii anavyowasilisha mawazo (Maudhui) yake.
Fani imejengwa na vipengele vifuatavyo;
- Wahusika
- Mandhari
- Muundo
- Mtindo
- Matumizi ya lugha
Wahusika
Hawa ni viumbe wanaotumika kufanya matendo katika kazi ya fasihi. Viumbe hawa huweza kuwa hai au wasio hai, halisi au wasohalisi. Hutumika katika kuwasilisha tabia za binadamu na maisha yake.
Tunaweza kuwaweka wahusika katika makundi mbalimbali kwa namna mbili ambazo ni kutokana na dhamira wanazobeba au kutokana na tabia zao (kifani).
Kutokana na dhamira tunapata
- wahusika wakuu na
- wahusika wasaidizi.
Mhusika Wakuu
Mhusika mkuu hutokea ytangia mwanzo hadi mwisho wa kazi ya fasihi.
Huyu ndiye hubeba wazo kuu katika kazi ya fasihi.
Wahusika Wasaidizi
Hawa ni wahusika ambao husaidia kuwaimarisha au kuwajenga zaidi wahusika wakuu. Pia, hubeba dhamira mbalimbali katika kazi ya fasihi.
Kutokana na tabia au matendo ya wahusika tunapata aina tatu za wahusika ambao ni;
- Wahusika mviringo/Duara
- Wahusika bapa
- Wahusika foili /shinda
Wahusika Mviringo
Ni wahusika ambao hubadilikabadilika kitabia, kimawazo au kimatendo kulingana na hali halisi ya maisha. Anaweza kuwa mtu mwema mwanzo na mwashoni akabadilika kuwa mtu mbaya au kinyume chake.
Wahusika Bapa
Ni wahusika ambao hawabadiliki kitabia, kimatendo wala kimawazo tangu mwanzo wa hadithi hadi mwisho. Kama ni mwanamapindizi hubaki hivyo tangu mwanzo hadi mwisho.
Wahusika Shinda/Foili
Ni wahusika ambao hawana msimamo. hubadilika kulingana na msukumo wanaoupata. Msukumo huo huweza kuwa ni mazingira au mhusika mwingine. Mahusika huyu hufanya matendo yake kwa sababu tu fulani amefanya. Hivyo, huweza kuwa mhusika mwema endapo atakuwa karibu na mhusika mwema au mbaya kwa sababu yupo na mhusika mbaya.
Kwa namna nyingine tunaweza kusema mhusika foili hana msimamo kwani hajui imani yake.
Mandhari
Ni mahali ambapo tukio hufanyika. Mandhari huweza kuwa halisi au ya kubuni.
Mandhari ya kubuni ni ile inayotengenezwa na mwandishi na si pahala halisi (hapafikiki wa kuonekana).
Mandhari halisi ni ile ambayo huweza kuthibitika kwani huweza kufikika na kuonekana kwani msanii huweza kutumia majina ya mji ya kweli.
Mtindo
Ni namna ya kipekee ya uwasilishaji wa kazi ya fasihi. Mwandishi huweza kutumia mitindo mbalimbali kama vile;
- Matumizi ya nafsi ya tatu, ya pili au ya kwanza.
- Matumizi ya barua.
- Matumizi ya semi kama vile; methali, misemo, nahau, n.k
- Matumizi ya hadithi simulizi.
- Matumizi ya nyimbo.
- Matumizi ya dayolojia
- Matumizi ya monolojia au
- masimulizi.
Muundo
Muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi. Muundo ndiyo huweza kutofautisha kama kazi hi ni riwaya, tamthiliya au ushairi. Kwa hiyo muundo hugusa mambo yafuatayo.
- Umbo la kazi ya fasihi kama ni tamthiliya, riwaya au ushairi.
- Idadi ya sura, beti au maonesho.
- Msuko wa matukio.
Kuna aina za mioundo kama ifuatavyo;
- Muundo wa moja kwa moja ni muundo ambao visa hupanya kwa mtiririko wa kisa cha mwanzo, kati mwisho. Pia huitwa muundo msago.
- Muundo rejea ni muundo ambao visa hupangwa kuanzia mwisho, kati, mwanzo au kati, mwanzo mwisho. Pia, huitwa muundo rejea.
- Muundo changamani ni muundo unaochanganya visa huweza kuanza mwanzo, kati mwisho na visa vingine huanzia mwisho, mwanzo na kudakia kati.
Matumizi ya Lugha
Ni namna msanii anavyotumia vionjo vya lugha katika kufikisha kazi yake kwa hadhira. Kwa mfano matumizi ya misemo, methali, tamathali za semi n.k.
Tamathali za Semi
Tashibiha
Huu ni ulinganifu wa vitu au hali mbili zinazotofautiana kwa kutumia maneno ya mlinganisho. Maneno ya mlinganisho ni kama; Kama vile, mithii ya, sawa na, kama n.k.
Kwa mfano;
- Anahema mithili ya fahali la n’gombe.
- Pua yake ni kama andazi.
Sitiari
Huu ni ulinganifu wa vitu tofauti bila ya kutumia maneno ya mlinganisho.
Kwa mfano;
- Elimu ni bahari
- Kibe na Mpaki ni chanda na pete.
Tashihisi
Ni mbinu inayohusu kuvipa sifa za kibinadamu viumbe visivyo binadamu.
Kwa mfano;
- Upepo ulipiga makofi.
- Anga lililia kwa huzuni.
Mubalaagha
Ni mbinu inayohusu uwekaji wa chuku nyingi ili kuonesha msisitizo wa kitu kinachosemwa.
Kwa mfano;
- Katika harusi ile walihudhuria watu elfu kwa maelfu.
- Mzigo ule ulikuwa mzito kama kichwa cha gari moshi.
Shitihizai/Kejeli
Mbinu hi hutumika kumaanisha kinyume na kisemwacho.
Kwa mfano mtu ambaye amevaa hovyo akaambiwa “ Kati ya wote wewe ndiye uliyependeza.”
Kijembe
Usemi huu hufanana kidogo na kejeli ila kijembe si kinyume.
Huu ni usemi wa mzunguko au wa kimafumbo unaokusudia kumsema mtu vibaya.
Kwa mfano, “Hakika utazaa mtoto mwenye pua ndefu.” Maneno haya anaambiwa mwanamke aliyetembea na padre wa Kiitaliano ambaye anafikiri ni siri.
Tasfida
Mbinu hii hupunguza ukali wa maneno ambayo ni marufuku kusemwa kwenye hadhara.
Kwa mfano;
- Mbadala wa neno amekufa ni amepoteza maisha.
- Mbadala wa neno chooni ni uani.
Lakabu
Ni mbinu inayobadilisha mpangilio wa kisarufi.
Kwa mfano, Jiwe lilinigonga nilipokuwa natembea bila viatu.
Tabaini
Huu ni usemi wa ukinzani unaolenga kutoa msisitizo.
Kwa mfano;
- Mrefu si mrefu, mfipi si mfupi.
- Mweupe si mweupe, mweusi si mweusi.
Mbinu Nyingine za Kisanaa
Takriri
Hii ni mbinu ya kurudiarudia maneno ili kuleta msisitizo.
Kwa mfano;
- Nasema sitaki, sitaki, sitaki kabisaaa!
- Unacheza cheza tu badala ya kusoma.
Tanakali Sauti/Onomatopeia/Mwigo sauti
Ni mbinu inayohusu kuiga sauti ya kitu fulani.
Kwa mfano; Mnyaaau!, Puuuh! Phtuu! n.k
Mdokezo
Ni mbinu ya kuanza kuelezea jambo bila ya kulimalizia.
Kwa mfano;
- Yaani ninge…….
- Walipokuwa peke yao waka……
Tashtiti
Ni mbinu ya kisanaa ambayo mhusika huuliza swali ambalo jibu lake analijua.
Kwa mfano; Unakula ugali (Wakati anaona anachokula)
Nidaa
Hii ni mbinu inayotumika kuonesha kushangaa kwa jambo. Mbinu hii huishia na alama ya mshangao.
Kwa mfano;
- Haaa! kumbe siyo yeye!
- Duuh! Alikula mbuzi mzima pekeyake!
Matumizi ya Ucheshi
Ucheshi hutumika pia ili kuifanya hadhira isichoke.
Matumizi ya Semi
Msanii huweza kutumia semi mbalimbali kama vile nahau, methali, misemo n.k.
Matumizi ya Lugha nyingine
Matumizi ya lugha za kigeni au za kimakabila pia huweza kuhusishwa ili kufikisha ujumbe au kuendana na uhalisia.
Matumizi ya Taswira (jazanda) na Ishara
Mbinu hii hutumika ili kufikisha ujumbe fulani kwa hadhira kusudiwa. Pia, hutumika ili kukwepa udhibiti.
Ishara
Ni jambo au kitu kinachosimama ili kuwasilisha jambo au kitu kingine.
Kwa mfano, neno simba linaweza kutumika kumaanisha ubabe au ushujaa.
Taswira
Ni picha inayojengeka akilini mwa hadhira. Kisawe cha taswira ni JAZANDA.
Ufuatao ni mfano wa taswira, “alivaa shati la bluu na suruali nyeupe iliyomfanya aonekane nadhifu.”
Kuna aina mbalimbali za taswira kama ifuatavyo
Taswira za Hisi
Hizi ni taswira zinazoibua hisia za hadhira kama vile woga, kinyaa, furahi, huzuni n.k
Taswira za Kufikirika
Hizi ni taswira zinazojenga picha zisizohalisi yaani zizoweza kuthibitika. Kama vile mbinguni, kuzimu, nchi ya ndani ya bahari n.k
Taswira zinazoonekana
Hizi ni taswira zinazothibitika kwani huakisi vitu vinavyojulikana.
Usikose makala yajayo yatayojikita katika kujadili vipengele vya kimaudhui.