Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Hadithi na masimulizi

Karibu tena katika makala zetu zinazoweza saidia wanafunzi wa kidato cha nne na wengineo. Leo tunajadili kuhusu hadithi za fasihi simulizi. Ambapo tutaona maana ya hadithi na vipera vyake pamoja na mifano ya hadithi hizo.

Hadithi ni nini?

Hii ni tanzu ya fasihi simulizi ambayo inahusisha masimulizi yaliyojengwa na visa pamoja na matukio mbalimbali. Hadithi huweza kuwa fupi au ndefu. Vivyo hivyo tanzu hii ina wahusika ambao ambao hubeba visa na matendo yamuwakilishayo mwanadamu. Wahusika wanaweza kuwa wanyama, binadamu, mimea, mizimu, miungu n.k.

Tanzu hii ina vipera vitano ambavyo ni: Soga, Tarihi, Visasili, Ngano na Vigano. Vipera hivi vinafafanuliwa kimoja baada ya kingine hapo chini.

SOGA

Hizi ni hadithi fupi zenye ucheshi ambazo zinasimuliwa kwa nia ya kufanya mzaha. Husimuliwa katika mtiririko wa matukio yenye kubeza. Pia, mara nyingi hutumika ili kuonesha tabia ya kijinga ya mtu au kabila.

Kwa mfano;

Wahehe Wala Mbwa

Wahehe ni kabila moja wapo linalopatikana katika mkoa wa Iringa. Kama ilivyo kwa makabila mengine, Wahehe wana vyakula vyao. Lakini wao hupenda zaidi kula nyama. Siku moja mzungu mgeni alipoteza mbwa wake. Alipokuwa anamtafuta, alikutana na familia mojawapo ya Wahehe wakimalizia kula chakula. Aliuliza kama wamemuona mbwa wake. Akasema “Did you see my dog around?” Wakawa hawamuelewi. Kwa sasa akaonesha vitendo “Did you see (huku akigusa macho) my dog around? (akinyooshea mazingira kidole).

Mmoja kati ya familia ile akaelewa labda mzungu anataka nyadogi (maharage). Akamwambia tumekula nyadogi akimuonesha kitendo cha kula. Mzungu baada ya kuona hayo alihuzunika akajua mbwa wake ameliwa na Wahehe. Akondoka akasambaza habari kuwa wahehe hula mbwa.

TARIHI

Hizi ni hadithi zinazosimulia zaidi kuhusiana na matukio ya kihistoria. Hadithi hizi husimulia matukio ya kweli yaliyotokea katika jamii. Kwa mfano hadithi za Kinjekitile Ngwale, Mkwawa, Bushiri n.k.

Kwa mfano;

Mwaka wa Ukame

Kiangazi kiliunguza kikaunguza. Mwaka huo sitausahau maana jua lilitoka lote bila kubakia. Basi siku moja wakati wa jua linawaka tukahamaki wingu kubwa jeusi linatokea Mashariki. Tukapata matumaini. Looh! kumbe ni balaa jipya – nzige. Wadudu wale uwasikie tu redioni. Omba usiwaone. Walitua kwenye mikuyu mtoni. Dakika tano, mikuyu ilikuwa vijiti. Hatimaye, Januari mwaka tisa mia hamsini na sita, mvua zilianza japo kwa maringo.

VISASILI

Hizi ni hadithi ambazo husimulia kuhusu asili ya kitu au jambo fulani. Hadithi hizi hubeba imani ya jamii fulani hasa kuhusu mwanzo wa ulimwengu, binadamu, tabia za wanyama n.k. Kwa mfano hadithi kuhusu ufupi wa mkia wa sungura, urefu wa shingo ya twiga n.k, mwisho wa hadithi hizi huishia “Hadi leo sungura ana……….”  

Tazama mfano ufuatao,                                                                                       

Ujumbe wa Mwezi

Siku moja Mwezi alimwita Kinyonga. Akamtuma kupeleka ujumbe muhimu kwa binadamu. Ujumbe ulikuwa “Kama nifavyo na kuishi tena, kwa hiyo nanyi mtakufa na kuishi tena.” Kinyonga akaanza safari mara moja. Miguu yake ilikuwa mifupi hivyo alitembea taratibu sana. Vivyo hivyo, alikuwa hawezi kuona vizuri kwa hiyo alipotea njia mara kwa mara.

Mara kinyonga akapitwa na sungura mdadisi. “Kwa nini uko mbali hivi na kwako?” “Unatafuta nini?” Sungura alimuuliza Kinyonga.  Kinyonga alikuwa amechoka sana lakini alifurahi kupata wa kuongea nae. Bila kufikiri, Kinyonga alimwambie Sungura ujumbe aliopewa na Mwezi kumfikishia Binadamu.

Sungura akamtakia Kinyonga safari njema kisha akakimbia. Akafikiri moyoni mwake “Nitaufikisha ujumbe huu mwenyewe. Utanipa utukufu na umaarufu kwa sababu ni ujumbe muhimu sana.”  Sungura pamoja na kuwa mjanja na mwenye kasi, lakini hakuwa na akili sana. Alivyokuwa anatembea aliurudiarudia ujumbe ili asisahau.

Mara Sungura akafika mahala ambapo Binadamu aliishi. Kwa majivuno akasema, “Binadamu, sikiliza kwa makini ujumbe kutoka kwa Mwezi, “Kama nifavyo na kupotea, pia nanyi mtakufa. Na hichi kifo kitakuwa ndiyo mwisho wenu.”   

Mwezi alisikia namna Sungura alivyopotosha ujumbe wake. Akakasirika sana. Akachukua fimbo na kumchapa kwa hasira Sungura usoni. Hii ndiyo sababu mpaka leo Sungura ana alama mdomoni na puani kwake.

Baada ya kitambo kidogo, Kinyonga alifika mahala Binadamu alipoishi. Akamweleza Binadamu ataishi tena baada ya kifo. Lakini Binadamu hakuwa na furaha kisha akajibu, “Umechelewa sana. Mwezi ametuambia ni lazima tufe.” Binadamu alimchukia sana Kinyonga na kumpiga. Ndiyo maana hadi leo Binadamu anamdharua na kumdharirisha Kinyonga. Na hii ndiyo sababu Kinyonga hujibadilisha rangi ili kumkwepa Binadamu.

NGANO

Hadithi hizi hujikita katika kuasa wanajamii kuhusu maadili ya jamii husika kwa kuwatumia mhusika mwema na mhusika mwovu. Pia, hadithi hizi huwa na wahusika ambao wana nguvu za ziada kuliko binadamu. Hivyo wahusika kama majini, mizimu na miungu huhusishwa. Mhusika binadamu ambaye anaenda kinyume na maadili ya jamii fulani huadhibiwa na mizimu lakini anayefuata maadili ya jamii husifika na hutunukiwa. Tazama mfanohapo chini..

Sinderela

Hapo zamani palitokea tajiri mmoja aliyekuwa na mke wake mgonjwa na mtoto wao wa pekee aliyeitwa Sinderela. Mama Sinderela, alipohisi kuwa muda wake wa kuishi umeisha, alimuita binti yake wa pekee  na kumwambia, “nikiondoka uwe mwenye heshima na kumcha Mungu. Sikuzote nitakulinda na nitakuwa nakutazama toka mbinguni.” Baada ya maneno hayo alifumba macho kisha akafa. Binti alimlilia mama yake siku zote. Alikuwa akienda kwenye kaburi lake kila siku na kulia.

Baba wa binti huyo alikuwa mtu mwenye kazi nyingi za kusafiri, hivyo alikuwa anamwacha binti peke yake. Baada ya muda tajiri huyo aliamua kuoa mke mwingine. Alioa mjane ambaye alikuwa na watoto wawili wa kike. Mjane pamoja na watoto wake hawakumpenda Sinderela. Walimfanya kijakazi.

Sinderela alikuwa akifanya kazi nyingi pale nyumbani ilhali watoto wa mama wa kambo walikuwa hawamsaidii kazi yoyote. Pamoja na kufanya kazi nyingi kama mtumwa, Sinderela hakuruhusiwa kula chakula mezani pamoja na ndugu zake. Alikuwa akila makombo yanayobaki baada ya mama wa kambo na binti zake kula. Pia, alikuwa analala jikoni. Sinderela alitandika mkeka chini wakati ndugu zake wakifurahia vitanda vyenye magodoro safi. Vivyo hivyo, Sinderela hakuwa akinunuliwa nguo nzuri.  

Panya na ndege walimwona Sinderela alivyokuwa akiteseka, walimuonea huruma kisha wakawa rafiki zake. Sinderela alikuwa akijiliwaza kwa kusikiliza ndege na Panya wakimuimbia.

Siku moja mfalme wa nchi ile aliamua kufanya kalamu kubwa. Hivyo aliwaalika watu wote washiriki katika kalamu ile. kalamu hiyo pia, ilikuwa kwa ajili ya mtoto wa mfalme kuchagua mke. Kwa hiyo mfalme aliagiza mabinti wote wahudhurie kalamu hiyo ili mtoto wake apate kujichagulia mke.

Mabinti walijiandaa na kuisubiri siku hiyo kwa hamu kubwa. Watoto wa mama wa kamambo nao walijaandaa. Mama wa kambo alitamani mmoja kati ya binti zake waolewe na mtoto wa mfalme. Mama huyo alimuamuru Sinderela awaandalie nguo nzuri watoto wake.

Siku ilipowadia Sinderela alitamani kujumuika na ndugu zake kwenda kwenye kalamu ya mfalme. Lakini mama wa Kambo alimzuia Sinderela na kumwambia kuwa yeye abaki nyumbani kwani hana nguo nzuri asije akawaaibisha.

Mama wa Kambo na binti zake walipoondoka. Sinderela akakumbuka kuwa kulikuwa na gauni la harusi ya mama yake alilolitunza. Akalitoa gauni hilo ili alivae aende kwenye kalamu. Lakini bahati mbaya gauni hilo lilikuwa limechanika. Akaanza kulishona huku akilia kwa kuhofia kuchelewa kwenye kalamu ya mfalme. Marafiki zake Panya na Ndege walikuwa wakibembeleza.

Ghafla akatokea bibi wa Sinderela na fimbo ya ajabu. Sinderela akashangaa na kumuuliza bibi huyo anataka nini? Bibi akamwambia, “nimekuja kukusaidia mjukuu wangu. Mimi ni bibi yako mzaa mama yako nimetoka mbinguni nije kukusaidia uende kwenye kalamu ya mfalme.” Sinderela akasema nawezaje? Maana sina nguo nzuri. Mara yule bibi akamgusa gauni la Sinderela kwa fimbo yake ya ajabu. Gauni lile likawa gauni zuri sana hakuna mfano. Kisha akagusa viatu vya Sinderela na fimbo yake ya ajabu. Viatu vya Sinderela vikawa viatu vizuri sijapata ona. Viatu hivyo vikawa vya kioo. Kisha akagusa boga, likageuka kuwa gari la farasi, akawagusa Panya wakabadilika na kuwa farasi na akamgusa Ndege akawa mwendesha farasi. Bibi akamwambia Sinderela panda uende kwenye kalamu ya mfalme lakini nguvu hizi zitaisha saa sita usiku. Hakikisha kabla ya saa sita usiku uwe umesharudi nyumbani.

Sinderela alipofika kwenye kalamu alikuta tayari sherehe imeanza. Alipoingia kila mtu alimshangaa kwa uzuri wake na jinsi alivyopendeza. Hata ndugu zake hawakumtabua ingawa yeye aliwatambua. Mtoto wa mfalme alimfuata Sinderela na kumuomba acheze nae. Sinderela alikubali. Walicheza kwa muda  mrefu na kila saa mtoto wa mfalme hakutaka kuondoa macho usoni pa Sinderela. Alijua kuwa amempenda sana binti huyo. Wakati wakiendelea kucheza, Sinderela alikumbuka maneno ya bibi yake. Alipoangalia saa ilikuwa ni saa sita kasoro dakika tano. Sinderela akamwambia mtoto wa mfalme lazima niondoke. Mtoto wa mfalme alitamani kumzuia lakini Sinderela aliponyoka na kukimbia. Wakati akishuka ngazi, mara kiatu chake kikachomoka. Hakuweza kukirudia maana mtoto wa mfalme alikuwa akimkimbiza. Sinderela akapanda kwenye gari la farasi akaondoka zake. Mtoto wa mfalme alikichukua kile kiatu na kusema nitamtafuta binti huyo popote alipo ili nimuoe.

Sinderela alipokaribia nyumbani zile nguvu ziliisha na akabadilika. Farasi wakawa Panya na mwendesha farasi akawa Ndege. Kisha gari la farasi likawa boga. Alipita njia za mkato na kufika nyumbani kwao. Baadae mama wa kambo na watoto wake walifika nyumbani wakihadithiana kuhusu mrembo aliyeonekana kwenye kalamu.

Baada ya siku, mtoto wa mfalme aliamua kuanza kumtafuta binti mwenye kile kiatu. alitembea na kiatu na kuingia kila nyumba akiwavalisha mabinti wa humo kiatu kile cha ajabu. Ajabu ni kuwa kila binti aliyekijaribu kiatu hakikuweza kumtosha. Walipofika nyumbani kwa kina Sinderela walimuita mama wa kambo na kumuuliza kama ana mabinti humo ndani. Mama akajibu kuwa alikuwa nao wawili. Alipowaita mabinti zake nao kiatu hakikuwaenea. Askari wa mtoto wa mfalme aliuliza kama kuna binti mwingine. Mama akajibu ni hao tu.

Mara askari akona mlango wa jikoni umefungwa. Akauliza mle kuna nini?Mama akajibu hamna kitu. Askari aliuelekea mlango ule na kuuvunja. Akamuona Sinderela amefungiwa humo. Akamwambia yakupasa ujaribu kile kiatu. Mama wa kambo akasema haiwezekani huyu binti hakuhudhuria kalamu ya mfalme. Lakini askari akamwambie kiatu hiki ni lazima kijaribiwe mabinti wote.

Sinderela alijaribu kiatu kile na kikamtosha. Mtoto wa mfalme alifurahi sana na akamkumbatia Sinderela na kuomba awe mke wake. Sinderela akakubali. Mara Bibi akatokea na fimbo yake. Akamgusa Sinderela kisha gauni lake likabadilika na kuwa zuri, Panya wakawa farasi na Ndege mwendesha farasi kisha boga likawa gari la farasi. Mtoto wa mfalme na Sinderela wakaondoka kuelekea kwenye kasri la mfalme.

Baadaye baba wa Sinderela alipewa taarifa na kuridhia mtoto wake aolewe na mtoto wa mfalme. Watu walimweleza Baba mambo aliyokuwa akiyafanya mama wa Kambo kwa Sinderela. Baba alikasirika sana na kuwafukuza nyumbani kwake. Sinderela na Mtoto wa mfalme wakaishi kwa raha katika kasri la kifalme.

VIGANO

Hizi ni hadithi ambazo hueleza kuhusu uovu wa watu kwa kusudi la kuadilisha. Mhusika mkuu huwa muovu, ambaye kutokana na uovu wake anapata madhara ama anatengwa na jamii au anakufa. Mara nyingi vigano huishia kwa semi (methali, nahau na  vitendawili ). Inaweza ikawa “Nimeamini mshika mawili, moja humponyoka”.  Tazama  Mfano hapo chini.

Tola Mchoyo

Hapo zamani za kale palitokea njaa kali katika kijiji cha mtakuja. Wanakijiji wa Mtakuja walisaidiana kwa chakula kidogo kilichopo ili wasiweze kufa kwa njaa. Tola alikuwa mwanakijiji wa Mtakuja. Tofauti na wenzake yeye alikuwa mchoyo sana. Alitangaza kuwa hana chakula kwa hiyo watoto wake walikuwa wanaenda kudowea kwa majirani kila mchana. Wakisha kula wanajifanya mama yao amewaita hivyo huaga na kuondoka.

Wanakijiji waliwazoea watoto wa Tola na tabia zao. Pamoja na hayo hawakuwafukuza kila walipokaribia chakula. Tola aliwaambia watoto wake kuwa nyumbani hamna chakula hivyo wakati wa usiku watoto walala na njaa. Lakini Tola alimwambia mke wake awe anamwandalia chakula kwa kificho na kukiweka mezani wakati watoto wamelala. Tabia ya Tola ikawa ni kula chakula gizani ili watoto wasimuone. Watoto walipolala, Tola alikaa mezani na kuanza kuwaimbia;

“Njaa ipo muda Mrefu

Watoto walala bila kula

Njaa ipo muda mrefu

Watoto walala bila kula

Mmmh! Mmmh! Mmmh!

Watoto walala bila kula

Siku moja wakati Tola akila gizani mara alitafuna kitu tofauti. Baada ya kikitoa akatambua kuwa ni konokono. Tola akaanza kutapika sana, alitapika mpaka nguvu zilimuishia. watoto walipowasha taa wakaona chakula mezani. Tola alipata aibu sana. Akawaomba msamaha watoto wake na kuwapa chakula. Tangu siku hiyo Tola aliacha uchoyo akawa anakula chakula pamoja na watoto wake. Ama kweli  “Njia ya mwongo ni fupi.”