Sunday, September 27Kiswahili kitukuzwe!

Ubantu wa Kiswahili

Kuna nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya Kiswahili. Moja ya nadharia hizo ni ile inayodai kuwa Kiswahili ni Kibantu. Nadharia hii inaegemea zaidi vigezo vya ulinganishi baina ya Kiswahili na lugha zingine za Kibantu. Vigezo hivyo huonesha mfanano wa Kiswahili na lugha za Kibantu kama vifuatavyo;

Kwanza ni mfanano wa msamiati wa msingi. Lugha ya Kiswahili na lugha zingine za Kibantu zimefanana sana katika msamiati hasa ule wa msingi. Kwa mfano; Neno la Kiswahili mwana linafanana na umwana (Kinyakyusa) na ng’wana – Kisukuma. Pia, neno jicho linafanana na iliso – Kizulu, eliiso – Kiruri, liso – Kisukuma na elisho – Kihaya. Mfanano huu unadhibitisha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kibantu.

Vivyo hivyo, vitenzi vya Kiswahili na vya lugha zingine za Kibantu vina miishilizio sawa. Irabu ya mwisho ya vitenzi vya Kiswahili na vya lugha zingine za Kibantu hufanana. Kwa mfano; Kitenzi chek-a (Kiswahili), sek-a (Kiruri) na thek-a (kikikuyu). Mifano hiyo inaonesha kuwa vitenzi vya Kiswahili na vya Kibantu huishilizia na irabu “a”.

Pamoja na hayo, lugha ya Kiswahili pamoja na lugha zingine za Kibantu huweka nomino zake katika ngeli. Kwa kutumia kigezo cha kimofolijia,  mfumo wa ngeli wa lugha ya Kiswahili hufanana na ule wa lugha zingine za Kibantu.

Si hivyo tu bali, mpangilio wa maneno katika sentensi za Kiswahili hufanana na mpangilio wa maneno katika sentensi za Kibantu. Kwa mfano; Katika Kiswahili sentensi; watoto wawili wanaoga ambapo (watoto ni nomino, wawili ni kivumishi, wanaoga ni kitenzi). Katika lugha ya Kingoni sentensi; vana bavili visamba ambapo (vana ni nomino, bavili ni kivumishi na bisamba ni kitenzi) na katika lugha ya Kizigua sentensi; wana waidi wahaka  ambapo (wana ni nomino, waidi ni kivumishi na wahaka ni kitenzi). Kutokana na mifano hiyo tunaona kuwa muundo wa sentensi za lugha ya Kiswahili kama ilivyo katika lugha zingine za Kibantu, huanza na nomino, kisha kivumishi ndipo kitenzi.

 Mwisho, lugha ya Kiswahili na lugha zingine za Kibantu zina mpangilio sawa wa sauti. Kwa mfano neno u/so – Kiswahili, u/bu/so – Kizulu, o/bu/so – Kiruri na bhu/so – Kisukuma. Hapa tunaona kuwa silabi za Kiswahili na silabi za ligha zingine za Kibantu ni silabi wazi kwani zote zinaishia na irabu.

Kwa ujumla, lugha ya Kiswahili na lugha zingine za Kibantu zinafanana katika vipengele hivyo kwa sababu zinatoka katika mzizi mmoja. Kwa hiyo, kutokana na vigezo hivyo, lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kibantu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *