Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Uandishi wa Hotuba

Karibu tena katika makala zetu za nukuu za kidato cha nne. Leo tutajadili kuhusu uandishi wa hotuba.

Hotuba ni nini?

Hotuba ni maelezo maalumu yanayotolewa na mtu mbele ya kundi la watu kwa madhumuni maalumu. Hotuba huweza kuwa za mafundisho au za taarifa. Hotuba za mafundisho ni kama vile; mahubiri au mawaidha, kampeni za kisiasa juu ya sera mbalimbali za vyama n.k. Hotuba za taarifa ni kama vile ripoti ya wizara au za kitaaluma.

Mambo ya kuzingatia wakati wa uandishi wa Hotuba.

  • Hotuba lazima ieleze ukweli kuhusu jambo au taarifa inayotolewa
  • Lugha fasaha itumike
  • Iwe imepangiliwa kimantiki
  • Iwapo kuna matumizi ya ishara lazima zitumike ipasavyo
  • Sauti ya mtoa hotuba lazima isikike

Muundo wa Hotuba

  • Utangulizi

Katika sehemu hii kuna salamu kwa jumla na kuwatambua watu muhimu kulingana na nyadhifa zao. Kuanzia wadhifa wa juu hadi wa chini.  Pia, kutoa shukrani kwa hadhira na kudokeza kiini cha hotuba hiyo.

  • Kiini

Hapa mtoa hotuba hutoa dhamira au ujumbe wa hotuba yake. Hueleza bayana makusudi ya hotuba yake kwa hadhira.

  • Hitimisho

Hapa huweza kueleza kwa ufupi yale yaliyozungumzwa, mapendekezo, suluhisho, maoni au changamoto.

Mfano wa Hotuba:

Kilimo motooo!!! Vijana juuuu!! Afyaa safiiii!!!

Ndugu mtendaji wa kijiji, mwenyekiti, wakulima, wanakijiji wote, mabibi na mabwana. Bwana Yesu asifiwe…, Asalaam aleikum…, Tumsifu Yesu Kristo….

Nina furaha kubwa kuzungumza nanyi leo hii. Jambo kubwa ni kuzungumzia mstakabali wa afya zetu kama wananchi. Wote tunajua kuwa, tunapatwa na magonjwa kutokana na ukosefu wa chakula bora. Hali hii inasababishwa na ukulima duni ambao hauzingatii kilimo cha mazao mbalimbali, utumiaji bora wa mbolea na kutozingatia ushauri wa wataalamu.

Kilimo hoyee!!…. Kutokana na changamoto hizo, serikali imewaletea wataalamu wa kilimo hapa kijijini ili muweze kulima kilimo bora kitakachosaidia afya zetu. Wataalamu hawa watafanya kazi pamoja nanyi ili kuhakikisha kila mkulima analima kwa tija na kunufaika na kilimo chake.

Sambamba na hilo serikali imeleta mbegu bora ambazo kila mkulima atanunua kwa bei ya punguzo. Mbegu hizi hupambana na magonjwa, pia huhimili hali ya ukame. Kwa hiyo, kwa kutumia mbegu hizi, tunategemea kila mkulima ataongeza mavuno yake.

Ndugu wananchi, tunatambua kuwa, mbegu bora bila mbolea si kitu. Hivyo basi, serikali imetoa punguzo kubwa katika bei ya mbolea. Kuanzia sasa mbolea itauzwa kwa nusu bei ya ile ya mwanzo. Kwa kufanya hivi tunajua kuwa wakulima mtavuna mazao mengi ambayo yatawaongezea chakula na ziada itakayouzwa ili mpate pesa ya kujikimu zaidi.

Pamoja na hayo, serikali itaanzisha shamba darasa ambalo kila mkulima anapaswa kuhudhuria ili ajue namna ya kulima kilimo mseto. Shamba hili litasimamiwa na wataalamu wetu wa kilimo. Kilimo mseto kitasaidia wakulima kuwa na chakula bora ambacho ni muhimu kwa afya zetu.

Natumia fursa hii kuwakumbusha kuwa, serikali imeshaonesha kwa vitendo umuhimu wa kilimo cha kisasa. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kuona wanachi wanawajibika katika nafasi zao. Wakulima wafanye juhudi katika ukulima wao na viongozi wawasimamie ili kufikia lengo la kustawisha chakula bora.  

Kilimo hoyee!!! Ndugu mtendaji, wakulima, na wananchi wote, nashukuru sana kwa kunisikiliza na nawatakia utekelezaji mwema.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *