Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Uandishi wa Risala

Karibu tena katikata makala zetu zinazohusu nukuu za kidato cha nne. Leo tajikita katika uandishi wa risala.

Risala ni nini?

Risala ni maelezo maalumu yanayotolewa na kikundi cha watu kwenda kwa mgeni rasmi. Pamoja na kuwa risala humlenga mgeni rasmi lakini lengo kuu huwa hadhira inayohusika kupata ujumbe. Mara nyingi risala husomwa katika matukio mbalimbali ya kijamii hasa sherehe.

Muundo wa Risala

  1. Kichwa cha Risala

Sehemu hii hutaja kusudi la risala na kikundi au wahusika walioandaa risala hiyo. Kichwa cha risala huandikwa kwa herufi kubwa, hupigiwa mstari au kukolezwa.  

  • Mwanzo wa risala

Sehemu hii ni utambulisho, humtaja mgeni rasmi, viongozi na halaiki kwa kuzingatia nyadhifa zao. Pia, hutaja madhumuni ya risala.

  • Kiini cha Risala

Hapa ndipo maudhui ya risala hutajwa. Kama ni mafanikio, changamoto na maoni kuhusu jambo husika.

  • Hitimisho

Hapa hutaja maoni, mapendekezo, rai mbalimbali za waandaaji wa risala hutolewa. Pia, shukrani hutolewa katika sehemu hii.

Mfano wa Risala

RISALA YA WAHITIMU WA KIDATO CHA NNE KWA MKUU WA WILAYA

Ndugu mgeni rasmi, ndugu mkurugenzi wa shule, Mwenyekiti wa bodi ya shule, wajumbe wa bodi ya shule, ndugu mkuu wa shule, makamu mkuu wa shule, mwalimu wa taaluma, mwalimu wa nidhamu, walimu wote, wafanyakazi wa shule, wazazi, wanafunzi, mabibi na mabwana, Shikamooni… Napenda kuwakaribisha sana katika mahafali haya ya tano katika shule ya sekondari Sisimba. Shule yetu ilianza mnamo mwaka 2014 ikiwa na wanafunzi 50 tu. Mpaka sasa shule hii ina wanafunzi 2010. Huku ikiwa na michepuo yote ya sayansi, sanaa na biashara.  

Ndugu mgeni rasmi katika kipindi chote hiki, wanafunzi, wazazi, walimu pamoja na wafanyakazi wengine wa shule hii wanashirikiana sana kwa lengo la kunyanyua kiwango cha taaluma. Ushirikiano huu umezaa matunda mazuri sana kwani tangia shule hii ianzishwe hadi sasa, hakuna mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne katika shule hii na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari ya juu yaani ya kidato cha tano.

Vivyo hivyo, pamoja na wafanyakazi wa shule, mkurugenzi, bodi ya shule na ofisi kuu wanahakikisha kuwa mwanafunzi haondoki na taaluma tu, bali akiwa amejengeka kinidhamu na kuwa mfano wa kuigwa. Jambo hili linafanya tujivunie shule yetu na kutamani kuendelea kuwepo.

Ndugu mgeni rasmi, shule yetu inatambua umuhimu wa michezo. Hivyo basi, wanafunzi pamoja na walimu wanashiriki michezo kwa ukamilifu. Kwa kuwa tunatambua kuwa michezo hujenga akili na fikra kwa mwanafunzi, shule yetu imeanzisha mashindano mbalimbali ndani ya shule na baina ya shule zingine. Jambo hili limefanya wanafunzi waweze kujifunza mambo mengi kutoka kwa wanafunzi wa shule zingine. Pia, imetia hamasa kwa wanafunzi kujifunza zaidi.

Vivyo hivyo, shule yetu ina maabara kubwa kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo. Maabara hizi ni za kemia, biolojia na fizikia. Kwa kupitia maabara hizi wanafunzi wamepata hamasa ya kusoma masomo ya sayansi pia zimewasaidia sana katika kufanya vizuri kwenye mtihani wao wa mwisho.

Ndugu mgeni rasmi, pamoja na mambo yote hayo, shule hii haijabaki nyuma katika kuwapeleka wanafunzi katika safari za mafunzo. Safari hizi huwasaidia wanafunzi kujifunza mambo mbalimbali nje ya darasa. Mafunzo hayo ni kama ya kihistoria, kijiografia na kisanaa. Safari hizi hufanyika katika makumbusho ya taifa, mbuga za wanyama na sehemu zingine kama hizo.

Ndugu mgeni rasmi, pamoja na mafanikio yote hayo, bado shule yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vitabu vya kiada na ziada, uhaba wa maktaba, uhaba wa walimu wa sayansi, uhaba wa vifaa vya michezo na uchakavu wa baadhi ya miundombinu. Pamoja na juhudi za uongozi wa shule bado mambo hayo yamekuwa changamoto. Hivyo basi tunaomba wadau mbalimbali waweze kutusaidia katika kukabiliana na changamoto hizi.

Ndugu mgeni rasmi, matarajio yetu ni kufaulu katika viwango vya juu. Pia, tunatamani shule hii iwe kituo bora cha kitaaluma na kinidhamu ili tuweze kujenga taifa bora lenye wananchi wenye elimu bora na wazalendo.  

Ndugu mgeni rasmi, wazazi, walimu na waalikwa wote, tunashukuru sana kwa kutusikiliza. Tunategemea mtakuwa nasi katika kuboresha shule yetu.

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *