Karibu tena katika mwendelezo wa makala zetu zanazohusu nukuu za kidato cha nne. Leo tutaangalia tanaendelea kujadili njia nyingine za uundaji wa maneno.
KUBADILI MPANGILIO WA MANENO
Njia hii huhusika katika ubadilishaji wa mpangilio wa herufi katika neno ili kuundwa neno jipya au maneno mapya. Mifano ifuatayo inaonesha hilo;
- Neno Imla linaweza kuwa; Mila, lima, mali au lami
- Neno tatu linaweza kuwa; tuta, utata au tatua
- Neno tiba linaweza kuwa; bati, tabia
- Neno kali linaweza kuwa; lika, alika, kalia
URUDUFISHAJI/URADIDI
Hii ni njia nyingine ya uundaji wa meneno ambapo neno jipya huundwa kwa kurudiarudia neno moja. Hapa nenio linalorudiwa ni neno amilifu yaani linalojitosheleza kimaana likiwa pekeyake. Tazama mifano ifuatayo:
- sawa →sawasawa
- mbali→ mbalimbali
- Pole→ Polepole
- Haraka→ Harakaharaka
- Taka → Takataka
- Vile →vilevile
- Moto→ motomoto
- Omba →ombaomba
- Bara →barabara
- Unyevu → unyevunyevu
UFUPISHAJI
Hii ni njia ya uundaji wa meneno mapya ambapo baadhi ya herufi katika maneno kuchukuliwa ili kuunda neno jipya. Kwa mfano;
- Upungufu wa Kinga Mwilini – UKIMWI
- Chama cha Mapinduzi – CCM
- Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA
- Taasisi ya Taaluma za Kiswahili – TATAKI
- Virusi Vya UKIMWI – VVU
- Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania – UKUTA
- Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa – MEMKWA
- Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania – MKURABITA n.k
Zingatia: Maneno mapya yanayoundwa kwa njia hii huandikwa kwa herufi kubwa.
UHULUTISHAJI
Njia hii huhusisha kitendo cha kuweka pamoja sehemu za maneno ili kuunda neno jipya. Tutazame mifano hapo chini.
- Chakula cha jioni – Chajio
- Hati za Kukataza – Hataza
- Delta kama Tao – Deltao
- Neno Rununu (kusikia sauti kutoa mbali) na Maninga (macho “Kingozi”) limekuwa – runinga
- Joto baridi – Jotoridi
- Mnyama mfu – Nyamafu
- Kizio geugeu – kiziogeo
- Mtu asiye kwao – msikwao
Uhulutishaji na ufupishaji hutofautiana kwa sababu uhulutishaji hujikita katika kuchukua sehemu ya neno lakini ufupishaji huchukua baadhi ya herufi za menono mbalimbali ili kuunda neno moja.
UKOPAJI
Hii ni njia ya kuunda maneno mapya kwa kuchukua maneno katika lugha moja na kuyaweka katika lugha husika bila ya kuyafanyia marekebisho ya kisarufi. Katika Kiswahili maneno yafuatayo ni ya mkopo;
- Ikulu (Kisukuma/Kinyamwezi)
- Shukrani (Kiarabu)
- Kitivo (Kipare/Kisambaa)
- ng’atuka (Kizanaki)
- Bunge (Kigogo)
- Dari (Kiajemi)
- Bandari (Kiajemi)
- Salaam (Kiarabu)
- Hela (Kijerumani)
- Laki (Kihindi)
UTOHOAJI
Hii ni njia ya kuchukua maneno kutoka katika lugha moja kisha kuyafanyia marekebisho ya kisarufi ili yaweze kutumika katika lugha husika. Kwa mfano maneno kama:
- Picture (Kiingereza) – Picha
- Shirt (Kiingereza) – Shati
- Caraco (Kireno) – Korosho
- Carta (Kireno) – Karata
- Lenco (Kireno) – Leso
- Darbyn (Kiajemi) – Darubini
- History (Kiingereza) – Historia
- Paisa (Kihindi) – Pesa
- Bughsha (Kituruki) – Bahasha
- Kohkoni (Kituruki) – Korokoroni
KUANGALIA KAZI YA KITU
Neno huweza kuundwa kwa kuangalia shughuli ya kitu husika. Kwa mfano;
- Chuja – Chujio
- Funika – mfuniko
- Futa – Mfuto
- Funga – Kifungo
- Bana – ubanio
- Fagio – ufagio
- Fungua – funguo
- Kokotoa – kikokotozi
- Shika – Mshikio
KUFANANISHA UMBO(SURA), TABIA AU SAUTI
Kufananisha Sauti
- Nyaau!! – nyau
- Pikipikipikipiki!! – pikipiki
- Tututututu!!!! – mtutu
- kukukuku!!! – kuku
Kufananisha Sura/Umbo
- Kifaru [dhana ya kivita imefananishwa na kifaru mnyama]
- Mkono wa tembo [aina ya ndizi imefananishwa na mkonge wa tembo]
- Mshale [aina ya ndizi iliyofananishwa na mshale “silaha ya jadi”]
- Kidole tumbo [sehemu ya utumbo inayofananishwa na kidole.]
- Pembetatu [umbo lenye pembe tatu]
Kufananisha Tabia
- Kifaurongo – mdudu anyejifanya kuwa amekufa ingali yuko hai.
- Kinukamito – mwanamume asiyedumu na wakeze.
Njia hizo hapo juu ni baadhi ya njia zinazotumika katika kuunda maneno mapya. Njia zingine zilifafanuliwa katika makala zilizopita.