Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Muhtasari wa Uchambuzi wa Diwani ya Malenga Wapya na Wasakatonge

Jina la Kitabu: Wasakatonge

Mwandishi: Mohammed S Khatibu

Utangulizi

Diwani hii imejikita katika kutetea tabaka la wasionacho. Tabaka hili linanyanyaswa, linakandamizwa na kuonewa na tabaka la walionacho. Kwa ujumla mwandishi anataka kujenga jamii mpya ambayo itakuwa na usawa na inayozingatia misingi ya haki.

MAUDHUI

Dhamira Kuu

Katika diwani hii tunapata dhamira kuu mbili ambazo ni;

 1. Ujenzi wa Jamii mpya na
 2. Ukombozi.

Ujenzi wa Jamii Mpya

Mwandishi anajadili ujenzi wa jamii mpya ambayo inatupilia mbali unyonyaji, unafiki, matabaka, uongozi mbaya na usaliti. Kwa hiyo mwandishi anaona kuwa tutaifikia jamii mpya kwa;

 1. Kupiga Vita Uongozi mbaya
 • Uongozi mbaya ni chanzo cha matatizo katika jamii. Uongozi mbaya hunyima wananchi haki na hukandamiza wanyonge. Jamii mpya ni lazima ijali misingi ya haki na usawa. Mambo haya yanazungumzwa katika shairi la “Madikteta” na shairi la “Unyama”.
 • Pia viongozi hujilimbikizia mali na kushika njia zote za uzalishaji mali huku wakimuacha mwananchi katika hali mbaya ya kimaisha. Haya yanaonekana katika shairi la “Miamba”. Kama haitoshi viongozi huwanyima watu uhuru wa kuzungumzia maovu yanayofanywa na viongozi hao. Hili linaonekana katika shairi la “Marufuku”
 • Vivyo hivyo, shairi la “Pepo bila kifo” linaonesha kuwa viongozi wabaya ni wale ambao hawawajibiki lakini wanapenda maisha ya anasa.

2. Kuwa na Demokrasia ya Kweli

Msanii anaona kuwa jamii mpya ni lazima iwe na demokrasia ya kweli. Serikali yenye demokrasia ya kweli hujali maslahi ya wananchi na kuwapa nafasi ya kwanza. Msanii anaonesha kuwa viongozi bado hawawajali wananchi. Mashairi kama “Madikteta”,Saddam Hussein” na “Unyama” yameweza kuonesha mambo hayo.

3. Kupiga Vita Ukoloni Mamboleo

Ukoloni mamboleo unapaswa kupigwa vita kwa sababu ni chanzo cha umasikini katika nchi zetu. Kutokana na ukoloni mamboleo rasilimali za nchi hunyonywa kwa kupitia migongo ya msaada. Mambo haya yanaonekana katika shairi la “Tiba Isiyotibu”, “Klabu” na “Hatuna Kauli”

4. Kupiga Vita Matabaka

Kwa kiasi kikubwa msanii ameonesha kuwa matabaka ni tatizo kubwa katika jamii. Matabaka hupelekea upotevu wa usawa katika jamii. Tabaka a chini marazote huonewa, hunyonywa na kukandamizwa. Mambo haya yanaonekana katika mashairi ya “Wasakatonge”, “Miamba” “Hatuna Kauli” na “Mvuja Jasho”.

5. Kupiga Vita Unafiki na Usaliti

Mshairi naonesha kuwa katika jamii viongozi wamejaa unafiki na usaliti. Viongozi hawa wanajifanya kuwa watakatifu kumbe wamejaa uovu mkubwa. Katika hili msanii amewagusa viongozi wa dini pamoja na wa serikali. Mambo haya yanaonekana katika shairi la “Wasodhambi”, “Vinyonga” na “Pepo bila Kifo”

6. Kupiga Vita Mmomonyoko wa Maadili

Msanii ameonesha kuwa jamii mpya ni ile ambayo inafuata maadili. Katika jamii zetu watu wanakiuka maadili na kufanya mambo ambayo hayastahimiliki. Katika shairi la “Jiwe si Mchi” msanii anakemea vitendo vya usagaji, Pia katika shairi la “Wewe Jiko la Shamba” msanii anakemea matendo ya umalaya.

Ukombozi

Msanii anaona kuwa jamii lazima ijikomboe ili iweze kuwa na maendeleo. Jamii lazima ijikomboe katika nyanja zifuatazo;

 1. Ukombozi wa Kisiasa

Msanii anaona kuwa jamii yetu inabidi ibadili misingi ya kisiasa ili iwe sehemu salama ya kuishi. Misingi hiyo ipige vita machafuko ya kisiasa, uharibifu wa mazingira na kuondoa umasikini. Mambo haya yanaonekana katika shairi la “Afrika”. Pia, katika shairi ya “Nuru ya Tumaini” mshairi anatamani kuona jamii ambayo imetupilia mbali dharau, kunyanyasika, ubaguzi na utawala wa mabavu.

 • Ukombozi wa Kiutamaduni
 • Mshairi anaonesha kuwa umefika wakati wa kutupilia mbali mila na desturi mbaya zinazomkandamiza mwanamke. Jambo hili linaonekana katika shairi la “Tohara” na shairi la “Mwanamke”
 • Pia, msanii ameonesha kuwa ni lazima wanawake waungane ili kupigania haki zao. Wanawake wanatakiwa kuwa wasomi, watu wasiosengenyana, wenyemadaraka na wazalishaji mali. Mambo haya yakifanyika mwanamke hawezi kukandamizwa. Hili linaonekana katika shairi la “Wanawake wa Afrika
 • Vivyo hivyo, msanii anaonesha kuwa wanawake ni lazima wafanye kazi kwa bidii  na kuachana na majungu, umbeya na ugomvi ili kujikwamua kiuchumi. Jambo hili linaonekana katika shairi la “Mama Ntiliye”
 • Ukombozi wa Kiuchumi

Msanii anaona kuwa jamii haiwezi kufikia hatamu ya usawa kama tabaka la chini halitajikomboa kiuchumi. Watu wa tabaka la chini ni lazima wafanye kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi. Mambo haya yanaonekana katika mashairi ya “Walala Hoi”, “Wasakatonge” na “Mvuja Jasho”

Pia, msanii anaonesha kuwa ili jamii zetu ziache kunyonywa ni lazima zijikomboe kiuchumi. Hivyo zitaepukana na misaada isiyo na tija. Mambo haya yanaonekana katika shairi la “Tiba Isiyotibu”

 • Ukombozi wa Kifikra

Msanii anaonesha kuwa fikra tegemezi ni chanzo cha kukandamizwa. Hivyo basi, tabaka la chini lazima lijikomboe kifra katika nyanja zote za kimaisha. Wanawake lazima washiriki katika shughuli za kiuchumi na jamii iache kutegemea misaada ya wahisani. Katika shairi la “Wanawake wa Afrika” na shairi la “Tiba Isiyotibu” yameoneshwa haya.

FANI

 1. Muundo

Msanii ametumia miundo changamani kama ifuatavyo:

 • Tahlitha katika mashairi; “Kansa”, Nilinde na “Jiwe si Mchi”
 • Tarbia katika mashairi; “Mahaba”, Mtemea Mate Mbinguni na “Mcheza hawi kiwete”
 • Takhmisa katika mashairi; Unyama, Fahali la Dunia na Bundi.

2. Mtindo

Msanii ametumia mitindo yote miwili ambao ni wa kimapokea na wa kisasa. Ingawa ametumia zaidi mtindo wa kisasa.

Kimapokeo kuna mashairi kama vile; Wewe Jiko la Shamba, Buzi Lisilochunika na Jiwe si Mchi

Mtindo wa kisasa umetumika katika mashairi kama; Tiba Isotibu, Tonge la Ugali na Madikteta.

3. Matumizi ya Lugha

Tashihisi

Katika shairi “Afrika” radi yenye chereko

Katika shairi “Tiba Isiyotibu” inaumwa Afrika

Katika shairi la “Miamba” chui na simba wanatamba

Sitiari

Uchoyo ni sumu katika shairi la “Pendo Tamu”

Mate si baraghum katika shairi la “Mtemea Mate Mbinguni”

Kuvua pono ni tusi katika shairi la Sivui Maji Mavu.

Tashibiha

Lanuka kama ng’onda katika shairi la “Kansa”

Chanda na pete kama udi na ambari katika shairi la “Nilinde”

Takriri

Hili buzi, buzi gani…. katika shairi la “Buzi Lisilochunika

Matumizi ya Ishara na Taswira

Nahodha – Viongozi ( shairi “Nahodha”)

Jahazi – Nchi (shairi “Nahodha”)

Vinyonga – wanafiki (shairi “Vinyonga”)

Jiko la shama – mwanamke malaya (shairi “Wewe Jiko la Shamba”)

Chui na simba – tabaka tawala ( shairi “Miamba”)

525 Comments