Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

MAENDELEO YA KISWAHILI

 1. UKUAJI NA UENEAJI WA KISWAHILI BAADA YA UHURU

Kutokana na umuhimu wake wakati wa ukombozi, lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa sana baada ya kupata uhuru. Serikali ilisaidia sana kukuza na kuenea Kiswahili baada ya uhuru kwa kufanya yafuatayo;

 1. Kiswahili Kupewa Hadhi ya Lugha ya Taifa

Baada ya uhuru serikali ilitangaza kuwa Kiswahili kitakuwa lugha ya taifa. Kwa kuwa lugha hii iliunganisha watu mbalimbali nchini haikuwa shida kupokelewa na wananchi wengi. Kutokana na hili, lugha ya Kiswahili ilianza kutumika bungeni, katika ofisi za serikali, kwenye mikutano ya kijiji, shughuli zote za kisiasa, shuleni, sokoni, kwenye biashara mbalimbali na kila kona ya nchi. Jambo hili liliwafanya wananchi wengi wajifunze Kiswahili.

 • Kiswahili Kutumika kama Lugha ya Kufundishia na Kama Somo la Lazima

Serikali ilitangaza Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika elimu ya shule za msingi. Pia, kama somo la lazima katika shule za sekondari. Hivyo basi, wanafunzi waliona umuhimu wa kujua lugha hii. Wakajifunza na kufanya Kiswahili kienee zaidi.

 • Kuanzisha Asasi Mbalimbali za Kukuza na Kueneza Kiswahili

Baada ya uhuru, serikali ilianzisha asasi mbalimbali za kukuza na kueneza Kiswahili. Asasi hizo zilishughulika kuandaa vitabu vya Kiswahili, kusanifisha lugha, kuongeza misamiati, kuhimiza watu waandike vitabu vya Kiswahili, tafsiri na kuandaa warsha na semina mbalimbali za Kiswahili.

 • Kuanzishwa kwa Taasisi ya  Elimu ya Watu Wazima

Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1963. Lengo kubwa lilikuwa kutoa fursa ya elimu kwa watu wazima waliokosa elimu katika umri mwafaka. Lugha inayotumiwa kufundishia ni lugha ya Kiswahili. Pia, masomo yalifundishwa kwa lugha ya Kiswahili. Taasisi hii imesaidia sana kueneza Kiswahili kwani watu wazima waolihitaji elimu hii, iliwapasa wajifunze lugha ya Kiswahili pia.

 • Vyombo vya Habari

Vyombo vya habari kama redio na magazeti vimesaidia sana kueneza Kiswahili. Vyombo hivi vinatoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kuwa huwafikia watu wengi kwa pamoja, vimetoa mchango mkubwa wa kusambaza na kueneza Kiswahili nchini na nje ya nchi. Vivyo hivyo, hata sasa kuna vyombo mbalimbali vya habari hususani redio na runinga za nje ya nchi ambavyo hutoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Mfano wa vyombo hivyo ni; BBC Swahili (London), Redio Deutche Welle (ujerumani), Redio Japan, Redio Sauti ya Amerika n.k. Jambo hili linarahisisha ueneaji wa Kiswahili duniani.

 • Asasi Mbalimbali Za Kukuza na Kueneza Kiswahili

Baada ya uhuru serikali ilianzisha asasi mbalimbali za kukuza na kueneza Kiswahili. Asasi hizo zina majukumu mbalimbali ambayo husaidia kukuza na kueneza Kiswahili. Asasi hizo ni kama zifuatazo;

 1. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) kwa sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI)

TATAKI

Mwaka 1963, Idara ya Lugha ya Afrika Mashariki ilihamishiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mnamo mwaka 1964 idara hiyo ilipandishwa hadhi na kuwa TUKI. Lengo kuu la taasisi hii ilikuwa ni kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki. Madhumuni zaidi ya TUKI ni kama yafuatayo;  

 • Kuendesha uchunguzi wa lugha Kiswahili ili kustawisha na kukuza lugha hii
 • Kuwatia moyo waandishi wa vitabu vya Kiswahili
 • Kukuza maneno ya Kiswahili na kuandaa kamusi
 • Kuhifadhi ufasaha wa Kiswahili
 • Kufanya tafsiri na ukalimani
 • Kufanya semina na warsha mbalimbali za Kiswahili
 • Kushirikiana na serikali na vikundi vingine vyenye kusudi la kukuza na kueneza Kiswahili.

2. Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Idara hii ilianishwa mwaka 1970. Ambapo ilifundisha taaluma za Kiswahili kwa kutumia Kiswahili. Hivyo kazi kubwa ya idara hii ilikuwa kuwaandaa walimu na wataalamu wa Kiswahili kuanzia ngazi ya shahada ili waweze kufundisha katika shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu.  

Hata hivyo mwaka 2009 Idara hii ilingana na TUKI na kuzaa TATAKI ambayo imechukua majukumu ya Idara hii na yale ya TUKI. Kwa hivyo basi kwa sasa hakuna Idara ya Kiswahili – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wala Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Bali kuna Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Kwa kuwa TATAKI ilichukua majukumu ya idara na yale ya taasisi, hivyo basi ili kufanikisha majukumu yake imeundwa na idara mbili ambazo ni;

 • Idara ya Lugha ya Kiswahili na Isimu (ILUKII)

Katika idara hii, isimu ya lugha huchunguzwa na kufundishwa kwa wanafunzi wenyeji na wageni.

 • Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji (IFAMU)

Katika idara hii fasihi ya Kiswahili huchunguzwa, pia masuala ya masoko ya kazi za Kiswahili hushughulikiwa pamoja na kusimamia uchapishaji wa kazi zote za Kiswahili

3. Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Baraza hili liliundwa mwaka 1967. Ambalo ni chombo kikuu cha serikali kinachosimamia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Kazi za baraza hili ni kama zifuatazo:

 • Kuratibu na kusimia asasi zote za ukuzaji wa Kiswahili pamoja na mawakala wote wanaojishughulisha na ukuzaji wa Kiswahili.
 • Kuratibu na kusimamia  maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini kote.
 • Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida nchini.
 • Kutafsiri na kufanya ukalimani kwa mashirika, serikali na asasi nyingine.
 • Uchapaji wa vitabu vya taaluma ya Kiswahili
 • Kuendesha na kusimamia tafiti mbalimbali za Kiswahili
 • Kuwashauri waandishi watumie Kiswahili fasaha
 • Kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili kwa vitabu vyote vya Kiswahili vinavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.

Ili kufanikisha mambo haya yote, BAKITA ina idara tano. Idara hizo ni kama zifuatazo;  

 • Idara ya Uhariri na Uchapishaji

Shughuli kubwa ya idara hii ni kutoa ushauri kwa waandishi, kuhariri miswaada ya vitabu, uchapishaji wa taarifa za BAKITA, kuratibu mashindano ya uandishi wa insha na kushiriki katika shughuli za tasnia ya vitabu.

 • Idara ya Lugha na Fasihi

Kazi ya idara hii ni kusimamia matumizi sahihi ya Kiswahili katika vyombo vya habari, kutoa ithibati ya matumizi sahihi ya Kiswahili katika vitabu vinavyokusudiwa kutumika shuleni, kuratibu matumizi na maendeleo ya Kiswahili mikoani, maeneo ya kazi na katika vikundi mbalimbali vya wapenzi wa Kiswahili. Pia, hufuatilia maendeleo ya matumizi ya Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi.  

 • Idara ya Tafsiri na Ukalimani

Kazi ya idara hii ni kutoa huduma ya tafsiri na ukalimani kwa lugha mbalimbali kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli mbalimbali. Pia, idara hii hupitia tafsiri zilizofanywa na asasi mbalimbali au watafsiri binafsi na kutoa ushauri kuhusu masuala ya ukalimani na tafsiri.

 • Idara ya Istilahi na Kamusi

Kazi ya idara hii ni kufanya utafiti wa istilahi zinazotakiwa kusanifiwa, kuandaa orodha ya istilahi zinazosanifiwa na kuandaa istilahi sanifu kwa ajili ya kuchapishwa.

Pia, idara hii hufuatilia matumizi sahihi ya istilahi zilizosanifiwa na kuandaa kamusi kwa ajili ya matumizi ya shule, asasi mbalimbali na kutoa maelezo ya istilahi kwa watu wanaohitaji.

 • Idara ya Uhusiano

Idara hii huhusika na kutangaza kazi na shughuli za BAKITA. Pia, hujihusiha na usimamiaji wa vipindi vya Kiswahili katika redio na runinga. Pamoja na kuimarisha uhusiano na vyombo vingine vya kueneza Kiswahil

4. Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, Zanzibar (TAKILUKI)

Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1979 na serikali ya Zanzibar. Shughuli kuu za Taasisi hii ni kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar. Ili kufanikisha jambo hilo, taasisi hii ina majukumu yafuatayo:

 • Kuratibu na kusimamia maendeleo ya Kiswahili Zanzibar.
 • Kuendesha mafunzo ya Kiswahili kwa wazawa na wageni.
 • Kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili
 • Kufanya utafiti wa Kiswahili katika nyanya zake zote (Isimu na Fasihi)
 • Kuandaa istilahi za taaluma mbalimbali
 • Kutoa huduma ya tafsiri na ukalimani
 • Kufundisha lugha za kigeni
 • Kuandika vitabu mbalimbali vya Kiswahili
 • Kuwashauri waandishi wa Kiswahili
 • Kuandaa semina na warsha mbalimbali za Kiswahili na
 • Kusimamia matumizi ya Kiswahili Sanifu katika vyombo vya habari.

5. Chama cha Kiswahili cha Afrika (CHAKA)

Chama hiki kiliundwa mwaka 1978, wazo la kuunda chama hiki lilishirikisha nchi nne, yaani Zambia, Msumbiji, Kenya na Tanzania. Wazo hili litokea wakati wa warsha ya Kiswahili iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Majukumu ya CHAKA ni kama yafuatayo;

 • Kuanzisha vyama vya Kiswahili katika kila nchi mwanachama.
 • Kuanzisha vituo mbalimbali vya utafiti katika nchi hizo kwa ajili ya kukusanya data na kuwakutanisha watafiti wa nchi husika.
 • Kusaidia utoaji wa mafunzo ya Kiswahili katika nchi mwanachama na kuandaa vifaa vya kufundishia kama vile; kamusi, vitabu, santuli au kanda za sauti.
 • Kuandika vitabu vya maarifa tofauti kwa Kiswahili ambapo lengo ni kuufikishia umma maarifa mbalimbali kama vile; kilimo, biashara, afya n.k.
 • Kuendesha semina na warsha mbalimbali za Kiswahili kwa wadau mbalimbali wakiwemo; waandishi, wakalimani, watafsiri, watangazaji, watumishi wa serikali n.k.
 • Kutafuta misaada mbalimbali ya hiari ambayo inaweza kusaidia katika kuendesha warsha na semina za ukuzaji wa Kiswahili na
 • Kuwatafutia misaada ya mafunzo wakuzaji wa Kiswahili wakiwemo waandishi, walimu, wakalimani na watafiti ili waweza kufikia malengo yao ya kukuza Kiswahili.

6. Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA)

Chama hiki kilianzishwa na Mathiasi Mnyampala mwaka 1965 kwa lengo la kukuza ushairi na Kiswahili kwa ujumla. Katika azma hii UKUTA huandaa semina na makongamano ya Kiswahili na kutunga kazi za kifasihi. Chama hiki kiliandika mashairi mbalimbali yakiwemo; Ngojera za UKUTA (cha kwanza na cha pili), Mashairi ya Azimio la Arusha na Mashairi ya Miaka Kumi ya Azimio la Arusha.

 • Chama cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Chama hiki kilianzishwa mwaka 1970 na wanafunzi wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo kubwa ni kukuza ari ya kupenda somo la Kiswahili na kuthamini lugha ya Kiswahili kwa ujumla. Katika juhudi zao hizo, jarida la Kiswahili la Kioo Cha Lugha likaanzishwa, ambalo lina makala mbalimbali za Kiswahili.

Mafanikio ya Asasi hizi za Kukuza na Kueneza Kiswahili

Vyombo hivi vimeweza kuchangia sana kukuza na kueneza Kiswahili hadi kufikia sasa. Mafanikio ya vyombo hivi ni pamoja na;

 • Kuchapisha vitabu vingi vya Kiswahili, ikiwemo Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
 • Kuendesha mafunzo ya Kiswahili na kuzalisha wataalamu wa Kiswahili kwa kiwango kikubwa.
 • Kueneza Kiswahili nje ya nchi na kutoa mafunzo ya Kiswahili kwa wageni.
 • Kuandaa istilahi mbalimbali za taaluma mbalimbali.
 • Kutoa mafunzo ya Kiswahili kwa viwango tofauti vya elimu.
 • Kutokana na juhudi za vyombo hivi Kiswahili kimeweza kuenea zaidi duniani na hata kuwa lugha mojawapo inayotumika katika vikao ya Umoja wa Afrika (AU). Pia, Kiswahili kinatumiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa kama vile, BBC Swahili (London), Redio Deutche Welle (ujerumani), Redio Japan, Redio Sauti ya Amerika n.k.
 • Kuibua amali mbalimbali za Kiswahili kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa. k.v; chimbuko la Kiswahili, sarufi ya Kiswahili, fasihi ya Kiswahili n.k.

Matatizo Yanayozikumba Asasi za Ukuzaji na Uenezaji wa Kiswahili

Pamoja na mafanikio makubwa ya asasi hizi, kuna chngamoto mbalibali zinazokabili asasi hizi. Changamoto hizo ni kama zifuatazo;

 • Vyombo hizi vinakabililiwa na upungufu wa wataalamu. Chanzo cha upungufu huu ni kwa sababu wataalamu wengi hukimbilia nje ya nchi ili wapate masilahi mazuri.
 • Kuna uhaba wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za ukuzaji na enezaji wa Kiswahili.
 • Taasisi hazina vyombo binafsi vya habari ambavyo vingeweza kutangaza na kuendesha shughuli zake. Hivyo taasisi zimeshindwa kuendesha vipindi mbalimbali ambavyo vingesaidia kukuza na kueneza Kiswahili. Kwani gharama za uendeshaji kwa kutumia vyombo binafsi ni za juu.
 • Baadhi ya taasisi hazina ofisi za kudumu.
 • Taasisi bado zina uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi hivyo, kutoa mafunzo kinadharia zaidi pasina vitendo.

Tathmini ya Maendeleo ya Kiswahili Baada ya Uhuru

Mafanikio

Baada ya uhuru, lugha ya Kiswahili imepata mafanikio makubwa sana kutokana na juhudi za ukuzaji na uenezaji wa lugha hii. Mafanikio hayo ni kama vile;

 1. Kiswahili kimekuwa lugha ya taifa, hivyo kutumika kama lugha rasmi katika shughuli zote za kiserikali.
 2. Kiswahili kimekuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi na somo la lazima katika ngazi ya sekondari.
 3. Kiswahili kimefanikiwa kutumika kimataifa na kama moja ya lugha ya Umoja wa nchi za Afrika. Pamoja na hayo, mataifa mbalimbali yanajifunza Kiswahili kwa sasa. Kwa mfano Japan, Marekani, Uingereza, China, Msumbiji, Zambia na Botswana.
 4. Lugha ya Kiswahili inatumika katika kufanya tafiti mbalimbali za viwango vya elimu ya juu.
 5. Vyombo vya habari vya kimataifa vinatumia Kiswahili katika matangazo yake.
 6. Kiswahili kimepata wadau na asasi mbalimbali za kukuza na kueneza lugha hii.

Changamoto

Pamoja na mafanikio ya Kiswahili baada ya uhuru bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili lugha hii. Changamoto hizo ni kama zifuatazo;

 1. Kuna matumizi ya Kiswahili potofu.  Upotoshwaji huu unatokana na matumizi ya mchanganyo lugha. Pia, unatokana na athari za lugha mama za wazungumzaji.
 2. Bado kuna tatizo la Kiswahili kutothaminiwa na baadhi ya wazungumzaji. Baadhi ya watu wanafikiri kuwa lugha yenye thamani sana ni Kiingereza. Hivyo, hupenda kuonesha kuwa wanajua Kiingereza.
 3. Pia, hakuna uwiano wa matumizi ya Kiswahili nchi nzima. Kwa mfano, kifaa kinachotiririsha maji, Tanzania bara huitwa bomba wakati Tanzania Visiwani huitwa mfereji.
 4. Kwa upande mwingine kuna tatizo la uhaba wa wataalamu na vyombo vya kufundishia.
 5. Kiswahili bado hakitumiki kama lugha ya kufundishia katika viwango vyote vya elimu. Jambo hili limeendelea kudidimiza Kiswahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *