Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

LAHAJA ZA KISWAHILI

Karibu tena katika makala zetu zinazoegemea nukuu za kidato cha nne. Leo tutajadili kuhusu lahaja za Kiswahili Sanifu.

Lahaja ni nini?

Lahaja ni uzungumzaji tofauti wa lugha moja. Lahaja za lugha moja hutofautiana kimatamshi, kimiundo na kimsamiati.  Hizi hutokea katika lugha yoyote yenye wazungumzaji wengi. Kiswahili ni moja kati ya lugha ambazo zina wazungumzaji wengi. Kutokana na hili lugha hii ina lahaja nyingi. Mfano wa lahaja za Kiswahili ni Kimtang’ata, Kingazija, Kimvita, Kigwana n.k.

AINA ZA LAHAJA

Lahaja zinaweza kugawanywa katika aina tatu ambazo ni:

 • Lahaja za Kijiografia / Kitarafa

Hizi ni lahaja ambazo hujinasibisha na mahali. Kutokana na lahaja hizi tunatambua mahali mtu atokako. Kwa mfano; Lahaja ya Kiunguja hupatikana Unguja, Kimgao – Kilwa, Kiamu – Lamu n.k.

 • Lahaja za Kijamii  

Hizi ni lahaja zinazotambulisha kundi la mtu katika jamii. Kutokana na hili tunaweza kumtambua mtu kama anatoka katika tabaka la juu au la chini, ana weredi gani (kama ni; mwalimu, daktari, mwanasheria n.k), mtu wa mjini au wa kijijini n.k.

 • Lahaja za mtindopeke/Lahaja za Nafsi

Hizi ni lahaja ambazo hutofautisha baina ya mtu mmoja na mwingine. Kwa kutumia lahaja hizi tunaweza kutambua sauti ya anayezungumza kama ni ya John au Samwel bila hata kuwatazama.

MAMBO YANAYOSABABISHA UTOKEAJI WA LAHAJA

Lahaja huweza kuchochewa na mambo mbalimbali kama yafuatayo;

 • Mwachano wa kijiografia

Mambo yanayoweza kusababisha mwachano wa kijiografia ni kama vile; milima mikubwa, misitu, mito, bahari n.k. Mwachano wa kijiografia huweza kupelekea jamii za lugha moja kutokuwa na muwasala. Hivyo basi, jamii zinazozungumza lugha moja zinapoachana kijiografia na kutokuwa na muwasala wa muda mrefu huweza kuibua lahaja za lugha hiyo. Hii inatokana na mabadiliko ya lugha yanayopatikana kwa kila jamii. Mabadiliko haya hutofautiana baina ya jamii hizo, kwani zinakuwa hazina mawasiliano.  

 • Mwachano wa kijamii

Endapo jamii zinazozungumza lugha moja zikatengana kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, hadhi na imani, lahaja zinaweza kuzaliwa. Jambo hili linaweza kutokea kwa sababu jamii hizo zitakuwa hazina muwasala mzuri, hivyo mabadiliko ya lugha yanayotokea katika jamii moja si lazima yawe sawia na ya jamii nyingine. Utofauti huo huzaa lahaja.

 • Mwingiliano wa kijamii

Lahaja huweza kutokea kwa sababu ya mwingiliano wa kijamii. Jamii zinazozungumza lugha moja zinapokuwa na mwingiliano na jamii za lugha nyingine hupokea athari za lugha hiyo. Athari hizo zinasababisha jamii moja kuwa na msamiati mpya ambao haupatikani katika jamii ya lugha sawa.

 • Utabaka

Utabaka katika jamii huweza kuzaa lahaja. Katika jamii tunaweza kupata lahaja za tabaka la juu na lahaja za tabaka la chini, lahaja za mjini na lahaja za kijijini, lahaja za kada mbalimbali n.k.

UMUHIMU WA LAHAJA KATIKA LUGHA

 • Ni chombo cha mawasiliano

Kwa kuwa lahaja ni lugha iliyokamilika, hutumika katika kupashana habari miongoni mwa wanajamii.

 • Hutambulisha jamii

Kwa kutumia lahaja tunaweza kuibaini jamii. Hivyo, kama mwanajamii anazungumza Kingozi tutajua kuwa anatoka eneo la Pate, Kama anatumia Kimtang’ata tutajua anatokea eneo la Pangani n.k.

 • Hukuza lugha Sanifu

Msamiati mpya wa lugha Sanifu hutolewa katika lahaja. Hivyo basi, mchango wa lahaja ni kuongeza msamiati mpya katika lugha Sanifu.

 • Hupamba lugha

Kwa kuwa wazungumzaji wa lahaja moja hutofautiana na wazungumzaji wa lahaja nyingine, mrindimo wa sauti hutofautiana. Jambo hili huwafanya wageni wafurahie namna watu wa lahaja fulani wanavyozungumza. Katika Kiswahili watu wa Mombasa, Tanga na Zanzibar hufurahisha kuwasikiliza namna wanavyozungumza Kiswahili.

 • Huhifadhi historia ya jamii

Lahaja zimebeba tunu ya lugha. Hivyo kwa wanaisimu ili kujua historia ya lugha fulani basi hurejelea lahaja za lugha hiyo. Jambo hili hufanyika kwani lahaja nyingi zinakuwa bado zina uasili wake. Kutokana na hilo, huweza kuelezea kiini cha lugha kwa urahisi.

Mifano ya Lahaja za Kiswahili

LAHAJA ENEO INAPOZUNGUMZWA MFANO WA MSAMIATI
Kingozi Pate Ima (simama), Pulika (sikia), Masi (maovu)
Kiunguja Unguja Mjini  
Kihadimu/Kimakunduchi Unguja  
Kitumbatu Unguja Kaskazini  
Kimrima Tanga/Pangani/Dar es Salaam/Rufiji/Vanga/Mafia  
Kimgao Kilwa Chichwa (Kichwa), Chikaanguka ( Kikaanguka)
Kipemba Pemba Ganja (siri), zinga (tafuta), tongoa (sema)
Kimtang’ata Tanga/Pangani Oka (choma), jekejeke (wasiwasi), munyu (chumvi), pweta (tafuta)
Kivumba Vanga (Kenya) Vara (pata), vira (pita), avwera (anataka)
Kimvita Mombasa Biti (bichi), Chanda(kidole), vyaa (zaa) Kitwa (kichwa), jimbi (jogoo), kwea (panda)
Kiamu Lamu Iwe (jiwe), mayani (majani), nana (bibi), simbo (fimbo)
Kipate Pate Fadhaa (haraka), kondo (vita), pija (piga), utuku (soko)
LAHAJA ENEO INAPOZUNGUMZWA MFANO WA MSAMIATI
Chimiini/Chimabalazi Somalia/Mogadishu Chala (Kidole), Shikilo (sikio), oloka (nenda)
Kingazija Komoro Mashobo (mikogo), byindua (pindua)
Kingwana Zaire Moya (moja), mayi (maji), nduku (ndugu), njila (njia)..

9 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *