Sunday, September 27Kiswahili kitukuzwe!

KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI

WAINGEREZA NA BAADA YA UHURU

 1. UKUAJI NA UENEAJI WA KISWAHILI KATIKA ENZI YA WAINGEREZA
Bendera ya Tanganyika katika utawala wa Mwingereza

Waingereza waliichukua Tanganyika chini ya utawala wa Wajerumani baada ya vita ya kwanza ya dunia mwaka 1918. Wakati huo Kiswahili kilikuwa kimeenea sana hata kufikia Kiwango cha kushinda matumizi ya lugha za kwanza nchini Tanganyika. Kutokana na jambo hilo, Waingereza hawakuwa na la kufanya ila kuendelea kutoka pale ambapo Wajerumani walipokuwa wameachia.  Kwa kuwa walitafuta urahisi wa kuwatawala Watanganyika, waliamua kutumia lugha moja inayotumiwa na wengi ili kuwapa elimu. Lugha hiyo ilikuwa Kiswahili. Kwa kufanya hivyo, walieneza na kukuza Kiswahili. Kwa namna hiyo, mambo yaliyosaidia kukuza na kueneza Kiswahili katika enzi ya Mwingereza yanajadiliwa hapo chini.

 1. Elimu

Katika utawala wa Waingereza shule mbalimbali za misheni zilianzishwa. Waingereza walilisisitiza elimu ya mwanzo ifundishwe kwa Kiswahili. Pia, mwaka 1925 kampuni ya uchapishaji (East African Literature Bureau [EALB]) iliundwa ili kuchapisha vitabu vya shule kwa lugha ya Kiswahili. Kutokana na hilo Watanganyika wengi waliopata elimu walijua Kiswahili. Vivyo hivyo, waliotaka elimu hiyo walihitajika kujua Kiswahili. 

 • Utawala

Waingereza walisisitiza sana matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za utawala wao. Waliwasisitiza machifu kujua Kiswahili ili iwe rahisi kutumiwa kiutawala. Vivyo hivyo, wafanyakazi wote wa serikali wa ngazi ya chini walitakiwa kujua Kiswahili kama kigezo kimojawapo cha kuajiiriwa. Hivyo basi, watanganyika wengi walijifunza Kiswahili. Pamoja na hayo, utawala wa Mwingereza ulipelekea misamiati kama hospitali, polisi, dereva, baiskeli, sigara n.k kuongezwa katika lugha ya Kiswahili.  

 • Shughuli za Kiuchumi

Kwa kuwa Waingereza walikuja kuitawala Tanganyika, walianzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi. Shughuli kuu ilikuwa ni kilimo cha mazao ya biashara. Mazao kama vile; karanga, tumbaku na pamba yalilimwa sehemu mbalimbali kama vile; Urambo, Shinyanga, Kongwa, Nachingwea, Sikonge, Songea n.k. Katika kufanikisha shughuli hizo, waliwaajiri vibarua walioitwa manamba. Manamba hawa walikuwa wametoka katika sehemu mbalimbali za Tanganyika (Tanzania ya sasa)na walikuwa ni watu wa makabila tofautitofauti. Kutokana na hilo, lugha kuu ya mawasiliano baina yao ilikuwa Kiswahili. Jambo hili lilifanya hata manamba wasiojua Kiswahili wajifunze lugha hii. Vivyo hivyo, waliporudi kwao hawakuacha kuitumia lugha hiyo. Na kwa kufanya hivyo waliieneza zaidi.

Pamoja na kilimo cha mazao ya biashara, waingereza walijishughulisha na uchimbaji wa madini na ujenzi wa reli. Shughuli ambazo huwakutanisha watu wengi. Watu hao walitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.

 • Usanifishaji wa Kiswahili

Mchango mkuu ambao Waingereza waliweza kuutoa katika Kiswahili ni usanifishaji. Kwa kuwa Kiswahili kina lahaja nyingi, Waingereza walitaka lugha hii itumike kwa namna moja kila pahala. Kwa hiyo, mwaka 1928 lahaja ya Kiunguja iliteuliwa na kusanifiwa. Kiswahili kilichosanifiwa kilitumiwa shuleni, katika vitabu vya ziada na kiada, katika vyombo vya habari na katika shughuli nyinginezo. Kwa sasa Kiswahili Sanifu kimeenea zaidi dunia. Yote haya yanatokana na juhudi za Mwingereza za mwaka 1928.

 • Uanzishaji wa Jeshi (King African Rifle [KAR])

Ili kuweza kuhakikisha usalama wa koloni lao, Waingereza walianzisha jeshi. Jeshi hilo lilikusanya Watanganyika kutoka katika makabila tofauti tofauti. Wanajeshi hao waliwasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, lugha hii ilipata mwanya wa kuenea kwani wale wasiyoijua walifanya jitihada za kujifunza.

 • Uanzishwaji wa Vyombo vya Habari

Kupitia vyombo vya habari vilivyoanzishwa na Mwingereza Kiswahili kiliweza kuenea kwa haraka zaidi. Magazeti yalikuwa yanachapishwa kwa lugha ya Kiswahili, pia redio ilikuwa ikirusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Jambo hili lilifanya umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuonekana hivyo basi wengi walijifunza lugha hii. Magazeti yaliyoanzishwa ni kama vile; Mwangaza (1923), Mamboleo (1923), Sauti ya Pwani (1954) na Kiongozi (1950). Pia Redio (1950) iliitwa Sauti ya Dar es Salaam kisha Sauti ya Tanganyika na ndiyo hii inayoitwa TBC FM kwa sasa.

 • Dini

Walipofika Tanganyika, Waingereza walieneza dini yao ya Kikristo kwa kutumia Kiswahili. Mahubiri na mafundisho ya Kikristo yalitolewa kwa lugha hii. Jambo hili lilifanya wamishionari kujifunza Kiswahili. Pia, wazawa waliotaka kujifunza dini hii iliwabidi wajifunze Kiswahili kwanza. 

 • Harakati za Kudai Uhuru

Kuanzia mwaka 1954 TANU ilipozaliwa, harakati za kudai uhuru zilianza. Harakati hizo ziliendeshwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Lugha hii ilitumika kama chombo cha kuwaunganisha Watanganyika. Pia kulikuwa na vikundi mbalimbali vya burudani ambavyo vilikuwa vikitumia Kiswahili ili kuhimiza watu wadai uhuru wao. Mambo haya yalichochea kuenea kwa Kiswahili nchini.

Tathmini ya Maendeleo ya Kiswahili katika Enzi ya Mwingereza

Pamoja na kuwa Waingereza walitoa mchango mkubwa sana katika kukuza na kueneza Kiswahili, lakini bado kulikuwa na changamoto zilizozuia lugha hii kuenea kwa haraka zaidi. Changamoto hizo ni kama zifuatazo;

 • Kutofundishwa kwa Kiswahili katika shule zote

Lugha ya Kiswahili ilifundishwa katika shule za watoto wa Kiafrika tu. Lugha hii haikutumika kufundishia katika shule za watoto wa Kizungu walioishi Tanganyika katika enzi hizo. Jambo hili lilifanya Kiswahili kienee kwa watoto wa kiafrika tu na kuwekewa mipaka.

 • Kutotumika kwa Kiswahili kama lugha ya Kufundishia katika Ngazi Zote

Kiswahili kilitumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi ya shule za msingi tu. Katika ngazi ya sekondari na kuendelea Kiswahili kilitumika kama somo. Jambo hili linadidimiza Kiswahili na kuonekana kama lugha ambayo haijitoshelezi katika kufundisha ngazi za elimu ya juu.

 • Kukosekana kwa Vyombo vya Kizalendo vya Kuendeleza Kiswahili

Katika kipindi cha Waingereza, vyombo vya kuendeleza Kiswahili vilikuwa chini ya Mwingereza (Inter-Territorial Language (Swahili) Committee na EALB) hata viongozi wa vyombo hivyo walikuwa Wazungu. Jambo hili lilifanya harakati za ukuzaji wa Kiswahili nchini zikose mtandao mpana.

 • Kushamiri kwa Kasumba ya Kuthamini Kiingereza

Wakati wa ukoloni wa Mwingereza, wananchi wengi walikuwa na kasumba ya kuthamini zaidi Kiingereza kuliko Kiswahili. Mtu aliyejua Kiingereza alionekana kama msomi na mtu mwenye maendeleo zaidi. Jambo hili lilifanya watu wengi wapende kujifunza zaidi Kiingereza kuliko Kiswahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *