Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Mzizi katika Kiswahili Sanifu

Dhana ya Mzizi

Karibu tena katika makala yetu ya sarufi ya Kiswahili sanifu. Katika makala haya tutajadili kuhusu dhana ya mzizi. Ambapo maana ya mzizi na aina za mzizi zitajadiliwa.

Nini maana ya mzizi? Mzizi una maanisha nini? Mzizi ni nini?

Mzizi ni sehemu ya neno ambayo haiwezi kuchanganuliwa zaidi bila kupoteza uamilifu wake. Kuchanganuliwa kunamaanisha kuondoa viambishi. Kwa hiyo ili tuweze kupata mzizi wa neno, tunapaswa kuondoa viambishi vyote ambavyo vyaweza kuwa awali, kati au tamati, kisha sehemu inayobaki ndiyo huitwa mzizi wa neno. Tazama mfano ufuatao;

  1. Kula > ku + l + a
  2. Mlo > m + l + o
  3. Mlaji > m + l + a + ji
  4. Ulaji > u + l + a + ji

Katika mfano huo tunaona sehemu ya neno ambayo haibadiliki ni “l“. Hivyo basi huo ndiyo mzizi wa maneno; kula, mlo, malaji na ulaji.

Aina za Mzizi

Kuna aina mbili za mzizi wa neno.Aina hizo ni mzizi huru na mzizi funge.

  1. Mzizi huru ni mzizi ambao unaweza kusimama peke yake na kuwa na uamilifu wa neno. Kwa mfano, godoro, simba, gari, shule, jembe, kalamu n.k. Maneno hayo yote ni mzizi kwani hayawezi kuchanganuliwa katika sehemu ndogo zaidi bila kupoteza uamilifu wake kimsingi.
  2. Mzizi funge ni mzizi ambao hauwezi kusimama peke yake na kuwa na uamilifu wa neno. Kwa mfano, l katika mlo, chez katika cheza, li katika lia n.k. Sehemu zilizoandikwa kwa herufi kozwa ni mzizi funge.

Kwa ujumla mzizi ni sehemu muhimu sana katika neno. Kwani kila lugha lazima iwe na mzizi wa neno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *