Friday, July 10Kiswahili kitukuzwe!

Hadithi: Mapisi

Karibu tena katika makala yetu yanazohusu fasihi. Leo tutajadili kuhusu kipera kimojawapo cha hadithi simulizi ambacho ni mapisi. Hapa tutaeleza kuhusu maana ya mapisi, dhima zake, sifa aina za kipera hiki.

Mapisi ni nini?

Mapisi ni kipera cha hadithi ambacho husimulia matukio ya kihistoria yaani habari za mambo ya kale. Mapisi hueleza matukio kama yalivyotukia bila ya kuweka chuku au kwa kuweka chuku au ubunifu ndani yake.

Dhima kubwa ya mapisi ni kutunza historia ya jamii fulani kuhusu matukio ya kishujaa au matukio maalumu yaliyoacha alama katika jamii husika.

Sifa za Mapisi

 • Hueleza matukio ya kihistoria.
 • Huwa na ukweli ndani yake.
 • Ni thibitivu, yaani mambo yanayoelezwa huweza kuthibitishwa.
 • Hutunza historia ya jamii.
 • Huweka kumbukumbu kuhusu kuhusu jamii ya watu fulani. Tangu mwanzo wao hadi kizazi cha sasa.
 • Hueleza matukio ya kishujaa ya wahenga.
 • Hueleza mapito ya watu mbalimbali.

Vipera vya Mapisi

Mapisi ina vipera kama vile; Kisakale, salua, tarihi, nasabu na shajari.

 1. Kisakale ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa jamii fulani yenye kuchanganya chuku na ukweli wa kihistoria. Kwa mfano, hadithi ya Lwanda Magere, Fumo Lyongo, Somsoni na Delila, Ngwanamalundi, Kinjekitile n.k.
 2. Salua ni masimulizi ya kihistoria ambayo hayawekwi chuku. Salua ni kweli tupu ya kihistoria ambayo hayataji tarehe.
 3. Tarihi ni masimulizi ya kihistoria ambayo huambatana na tarehe zake. Kipera hiki huwekwa zaidi katika maandishi. Kwa mfano hadithi za ukombozi wa Tanganyika.
 4. Nasabu ni masimulizi ambayo yamejaa orodha ya wazee au wahenga wa mtu, yaani baba, babu, mama, bibi na wengine waliotangulia. Kwa mfano; Ibrahim akamzaa Isaka, Isaka akamzaa Yakobo, Yakobo akamzaa Yuda, Yuda akamzaa Peresi…..(mfano kutoka katika Biblia Takatifu). Nasabu hueleza kweli tupu. Dhima kuu ya nasabu ni kujenga mshikamano katika ukoo na ni sehemu ya tambiko ili wahenga watoe msaada kwa vizalia wao katika raha na shida ziwakumbazo.
 5. Shajari ni masimulizi ya kumbukumbu yanayomhusu mtu binafsi. Shajari husimulia kuhusu matendo na mapito ya mtu fulani ingawa si lazima awe shujaa au mhenga kama ilivyo kwenye kisa kale.

Kwa ujumla mapisi ni kipera amacho kimeingizwa kwenye maandishi kwani hutunza historia ya jamii nyingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *