Sunday, September 27Kiswahili kitukuzwe!

Hadithi: Kisasili

Karibu tena katika makala zetu za fasihi. Leo tutajadili kuhusu kipera kimojawapo cha hadithi simulizi ambacho ni Kisasili. Kwa hiyo tutaangalia maana, sifa na aina mbalimbali za visasili.

Kisasili ni nini?

Kisasili ni hadithi ya kale yenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, asili ya jamii yenyewe na watu wake na maana ya maisha yao na vyote hivyo huaminika kuwa ni kweli tupu na huambatana na miviga (matendo ya kimila).

Dhima kubwa ya kisasili ni kutetea imani ya kiroho inayofuatwa na na jamii. Kwa hiyo, kila jamii ina kisasili chake kinachoeleza kuhusu asili, chimbuko na mustakabali wa maisha yao. Jambo kubwa la kuweka wazi hapa ni kuwa kisasili huambatana na imani ya jamii na ya mtu mmoja mmoja. Imani ile ambayo uliapa kuilinda na kuifia ni kisasili. Tazama sifa za kisasili hapo chini.

Sifa za Kisasili

  • Hueleza kuhusu asili ya mambo yanayominika na jamii kuwa ni kweli tupu. Kwa mfano, mwanzo wa ulimwengu, mwanzo wa binadamu, asili ya uovu, wema, n.k.
  • Kisasili hubeba imani kuhusu asili ya ulimwengu na watu.
  • Kisasili huhalalisha desturi ya jamii fulani.
  • Kisasili hakibadiliki toka kizazi kimoja hadi kingine hudumu na asili yake.
  • Kisasili hutambulisha imani ya jamii husika.

Aina za Visasili

Kwa mujibu wa Mulokozi kuna aina tatu za visasili. Aina hizo ni; Kisasili cha usuli, kisasili cha ibada na dini na kisasili cha miungu na mizimu.

  1. Kisasili cha usuli kinaeleza asili au chimbuko la taifa au jamii fulani au wanadamu kwa ujumla. Katika aina hii kuna imani mbalimbai zinaibuka ambazo huzaa aina za kisasili cha usuli. Aina hizo ni; Kisasili cha usuli ombwe, kisasili cha usuli mvurugo, kisasili cha usuli wazazi wa ulimwengu, kisasili cha usuli mpigambizi na kisasili cha usuli utokeaji.
  2. Kisasili cha ibada na dini hueleza ni asili ya matendo ya kiibada. Namna ya kusali, kutoa sadaka au kafara, elekeo wakati wa ibada n.k
  3. Kisasili cha miungu na Mizimu hueleza asili ya matendo ya miungu. Kwa nini mungu fulani ana hasira kali, hapendi matendo fulani n.k.

Kwa ujumla kisasili ni masimulizi yanoaminika kuwa ni ya kweli na hurithishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya masimulizi. Na hasa husimuliwa na watu wazima ili yisichukuliwe kuwa ni mzaha wa kiubinifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *