Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Tanzu za Fasihi Simulizi

Karibu tena katika mwendelezo wa mjadala kuhusu fasihi. Leo tutajadili kuhusiana na kumbo za fasihi simulizi. Pamoja na kuwa wengi wamezoea kugawanya fasihi simulizi katika makundi manne yaani; Hadithi, Ushairi, Semi na Sanaa za Maonesho, katika mjadala wetu tutaenda zaidi ya hapo.

Kwa kumrejelea Mulokozi katika kitabu cha Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili (2017), tunapata kumbo nane za fasihi simulizi. Kumbo hizo ni; Semi, Nyambi, Maombi, Hadithi, Maigizo, Ushairi, Maghani na Ngomezi. Kumbo hizi zimegawanywa kwa kuzingatia vigezo vifuatayo;

 1. Umbile na tabia ya kazi.
 2. Muktadha wa uwasilishwaji au utendaji wake.
 3. Namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira.
 4. Dhima ya kazi hiyo kwa jamii.

Kwa kifupi tuangalie maana ya kumbo hizo kama zinavyofafanuliwa hapo chini.

 1. Semi ni utungo au kauli fupi za kisanaa zenye kubeba maana na hutoa funzo kwa jamii.
 2. Nyambi (Umoja: wambi ) ni mazungumzo ya mdomo juu ya jambo lolote lenye usanii ndani yake. Kwa mfano hotuba, malumbano ya watani, maombi na mizaha
 3. Maombi ni tungo zinazohusu mawasiliano na miungu, mizimu au Mungu.
 4. Hadithi ni utanzu wenye masimulizi ndani yake na hujengwa na lugha ya mjazo.
 5. Maigizo ni sanaa inayotumia watendaji ili kuiga matendo na tabia za watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kuelimisha.
 6. Ushairi/Nyimbo: Ushairi ni sanaa ya lugha ya mkato inayosawiri na kueleza jambo kwa namna ya kuvuta hisia na yenye unidhumu ndani yake. Wimbo ni utungo wa kisanaa unaowasilishwa kimuziki kwa kutumia sauti iliyo katika mpangilio fulani wa mahadhi na melodia na yenye mapigo ya kiurari.
 7. Maghani ni tungo za ushairi simulizi zinazofuata arudhi fulani na ambazo hutambwa kwa utaratibu wa uchanganyaji wa uimbaji na usemaji.
 8. Ngomezi ni fasihi simulizi inayowakilishwa kwa kutumia mlio au mdundo wa ngoma badala ya mdomo. Ishara za ngoma zinazotumika huiga misemo, tamathali na viimbo vya usemaji.

Pamoja na kuwa, tunaona marekebisho makubwa aliyoyafanya Mulokozi katika kugawa kumbo za fasihi simulizi. Hata hivyo, utenganishwaji wa maghani na ushairi si sawa. Pia, maombi huweza kuingizwa katika kumbo la nyambi. Kwa hiyo, kwa maoni yetu kwa kutumia vigezo vile vile alivyotumia mwanafasihi huyu tunaweza kuwa na kumbo sita za fasihi simulizi ambazo ni; Semi, Nyambi, Hadithi, Maigizo, Ushairi na Ngomezi. Kumbo hizi zitafafanuliwa moja baada nyingine sehemu inayofuata.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *