Sunday, September 27Kiswahili kitukuzwe!

Semi 1

Karibu kwenye mwendelezo wa makala zetu zinazohusu fasihi ya Kiswahili. Katika makala haya tutajadili kuhusu semi kama kumbo mojawapo ya fasihi simulizi. Semi ni uwingi wa neno usemi. Kama ilivyojadiliwa katika makala yaliyopita, usemi ni kauli fupi za kisanaa zilizobeba maana na ujumbe kwa jamii fulani.

Maana ya Semi

Semi ni kauli fupi za kisanaa zilizobeba maana na ujumbe kwa jamii fulani. Kwa mfano; Samaki mkunje angali mbichi, mwenda pole hajikwai, mpanda ngazi hushuka, kuku wangu ametagia mibani, wazungu wawili wachungula dirishani na elimu ni bahari.

Tanzu za Semi

Semi ina tanzu zifutazo;

 1. Methali
 2. Vitendawili
 3. Mafumbo na
 4. Misemo

1. Methali

Methali ni usemi mfupi uliojaa busara ndani yake na unaodokeza mafunzo mazito yaliyotokana na tajriba ya jamii husika. Tazamz mifano ya methali hapo chini.

 1. Haba na haba hujaza kibaba .(Methali hii hufundisha uwekaji wa akiba kidogo kidogo kwa ajili ya matumizi makubwa ya baadaye.)
 2. Haraka haraka haina baraka. (Methali hii hufundisha kutofanya mambo kwa pupa kwani mwisho wake huwa mbaya.)
 3. Juhudi si kupata, kupata ni majaaliwa ( Methali hii hufundisha kuwa pamoja na juhudi tunazoweka ni lazima tumtegemee muumba.)
 4. Mwenda pole hajikwai. (Maana ya methali hii ni sawa na ile ya mfano na. 2)
 5. Samaki mmoja akioza, wote wameoza. (Maana ya methali hii ni kuwa mtu mmoja aliye katika kundi akifanya ubaya basi kundi zima huhesabiwa ubaya.)

Kuna wakati mwingine mathali huonekana kama zinakinzana. Tazama mifano ifuatayo;

 1. Mvumilivu hula mbivu na Ngoja ngoja huumiza matumbo.
 2. Damu nzito kuliko maji na Heri jirani karibu kuliko ndugu mbali.
 3. Penye wengi hapaharibiki neno na Wapishi wengi huharibu mchuzi.
 4. Umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu na Heshima ya pweke kubwa.
 5. Chelewa chelewa utakuta mwana si wako na Haraka haraka haina baraka.

Kutokana na mifano hapo juu, tunaona kuwa methali hukinzana wakati mwingine. Lakini ukweli ni kuwa methali hutumika kulingana na mazingira husika. Hii ina maana kuwa, methali fulani itatumika kulingana na tukio la wakati huo na humlenga nani.

Hata hivyo kuna wakati mwingine methali hutumika kama chombo cha kiitikadi. Watawala huweza kutumia methali ili kuwakatisha tamaa watawaliwa. Kwa mfano methali “Mnyonge kupata haki ni mwenye nguvu kupenda”. Methali hii inamaanisha mtawaliwa hana haki mbele ya mtawala. Pia, watawaliwa huweza kutumia methali ili kuwaasa watawala wakumbuke kuwa cheo ni thamana tu. Mfano methali “Jumbe ni watu si kilemba” humaanisha pasipo watu hakuna mtawala kwa hiyo mtawala anaweza kuondolewa kwa nguvu ya umma.

2. Vitendawili

Vitendawili ni usemi ulio na swali ambalo huhitaji kufumbuliwa na hadhira. Semi hizi huwa na upande wa muulizaji na upande wa mtoa jibu. Endapo jibu halitakuwa sahihi au muulizwaji akashindwa kupata jibu, basi muulizaji hupewa mji ili ajibu swali hilo.

Pia, kitendawili kina mianzo ya kifomula. Mianzo hii hutumika kuiandaa hadhira.

Muulizaji husema; Kitendawiliiii!

Hadhir hujibu; Tegaaa!

Kisha kitendawili hutajwa na kutolewa jibu. Ndipo, muulizaji husema mtoa jibu kama amepata au amekosa.

Tutazame mifano ya vitendawili hapo chini. Majibu yataandikwa kwenye mabano.

 1. Wanangu wawili hushabihiana. [ Tui na maziwa au Utomvu na maziwa au Majivu na unga]
 2. Kuku wangu ametagia miibani. [ Nanasi].
 3. Blanketi la babu lina chawa. [Mbingu na nyota]
 4. Nyumba yangu ina nguzo moja. [Uyoga]
 5. Popo mbili zavuka mto. [Macho]
 6. Ameingia shimoni akiwa uchi, akatoka akiwa amevaa nguo nzuri.[Mbegu]

Kwa ujumla vitendawili huwafunza watu kuhusu mazingira yao, huburudisha akili na huchemsha bongo. Sanaa hii hutegemea uwezo wa mtu wa kung’amua mambo na kufananisha vitu katika mazingira yanayomzunguka.

Katika makala yafuatayo yatajadili kuhusu mafumbo na misemo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *