Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Semi 2

Karibu tena katika makala zetu zinazohusu fasihi. Katika makala haya tutajadili kuhusu tanzu zingine za semi ambazo ni mafumbo na misemo. Tazu hizi zitajadiliwa moja baada ya nyingine kama ifuatavyo;

3. Mafumbo

Mafumbo ni semi zilizofichwa maana ili zifichuliwe au ziwekwe wazi. Mafumbo huweza kuwa; chemsha bongo, fumbo jina, tabaini/vitatanishi mara nyingine huitwa mizungu.

Chemsha bongo ni maswali ambayo yanahitaji tafakuri ili kuyajibu. Baadhi ya maswali hayo ni ya kimapokeo lakini mengine hubuniwa na msemaji kwa kuilenga hadhira fulani. Kwa mfano, mbele ya bata kuna bata nyuma ya bata kuna bata. Je kuna bata wangapi?

Tabaini/Mizungu/Vitatanishi ni semi za ukinzani zinazokusudia kutoa ujumbe fulani. Kwa mfano, mweupe si mweupe, mweusi si mweusi, mkimbizi asiyekimbia.

Fumbo jina ni majina ya vitu au watu ambayo hubeba ujumbe fulani. Kwa mfano, jinti, Mwamvita, Kirukanjia n.k.

4. Misemo

Misemo ni semi zinazoibuka katika kipindi fulani na hubadilika au hutoweka au kubakia katika kumbukumbu ya watu kwa muda mrefu. Kategoria za misemo ni; simo, vitanzandini (vitate), tauria na nfumu. Tazama moja baada yan nyingine hapo chini.

Simo (misimu) ni ni semi za muda na mahali maalumu ambazo huzuka nakutoweka. Semi hizi huficha maana ili kutoa ujumbe fulani. Kwa mfano neno “utandawizi” (neno la kukejeli utandawazi), nguvu ya soda, chakachua n.k. Hata hivyo, simo zikipata mashiko makubwa hubakia katika jamii na kuwa nahau.

Nahau ni miongoni mwa simo/misimu iliyoweka mizizi katika jamii. Nahau hutumia lugha ya picha yenye fumbo ili kutoa ujumbe. kwa mfano; mkono wa birika, amepata jiko, amevaa miwani, mkono mrefu n.k.

Vitate ni ni kauli yenye mfuatano wa maneno yanayotatanisha kutamka. Husaidia kukuza matashi na kukuza msamiati. Huu ni chezo ambao mtu hutakiwa kutamka maneno hayo harakharaka au kwa kurudiarudia. Kwa mfano; Kafa Manzese mazishi Sinza. Kipi, kikusikitishacho? Waache wale wanawali wawili wale wali wao.

Tauria ni semi zenye kuchezesha maneno au sauti zinazofanana. Kwa mfano, Vipele namba vipele, vipele vipelelezi, vipelelezi si vile, si vile visivyo kazi.

Nfumu ni maelezo fafanuzi yenye kutumia mifano bunifu ili kutoa ujumbe kwa maana yenye ushawishi au hata kuchekesha. Kwa mfano, Chura aliwaambia waliofuatana nae “Mzigo wa mawe ya chuma huwa mzito” Wakamwuuliza “Ulishawahi kuubeba?” Akawajibu “Nilishawahi kukanywangwa na mtu aliyekuwa ameubeba.”

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *