Sunday, September 27Kiswahili kitukuzwe!

AINA ZA FASIHI

Karibu tena katika mwendelezo wetu wa mada za fasihi ya Kiswahili. Leo tutajadili kuhusu aina za fasihi na sifa za kila moja.

Kuna aina mbili za fasihi ambazo ni; Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi. Aina hizi zinajadiliwa moja baada ya nyingine sehemu inayofuata.

FASIHI SIMULIZI

Fasihi Simulizi ni fasihi itumiayo lugha ya masimulizi ya mdomo ili kufikisha ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Kabla ya maendeleo na mabadiliko mbalimbali ya uhifadhi, fasihi hii haikuwekwa katika maandishi. Hata hivyo, kutokana na ukuaji wa kiteknolojia na mabadiliko mbalimbali ya kiuhifadhi, fasihi hii haiwezi kutambuliwa tu kwa kuegemea masimulizi ya mdomo bali kwa kuangalia sifa zingine za kifasihi simulizi hasa hasa mianzo na miisho ya kifomula, matumizi ya wahusika wa fasihi simulizi n.k.

Ukweli ni kuwa, tunapoongelea usimulizi si lazima uwe wa mdomo tu. Usimulizi waweza kuwa wa kimaandishi au wa kimdomo. Kwa hiyo ni rai yetu kuwa, wakati wa kufasili maana ya Fasihi Simulizi lazima umakini uwepo.

SIFA ZA FASIHI SIMULIZI

  1. Fasihi simulizi ilianza kabla binadamu hajagundua maandishi. Ilianza ili kumliwaza binadamu alipokuwa akifanya kazi. Baadae ikawa ni mojawapo ya starehe ya binadamu huyo. Kwa maana hiyo, fasihi hii ni kongwe kuliko fasihi andishi.
  2. Fasihi simulizi huhifadhiwa kichwani kutokana na kurithishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Hata hivyo, mabadiliko yalitokea katika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi ili zisiweze kusahaulika kirahisi. Hivyo basi kazi hizo huhifadhiwa; Kimaandishi kwenye ngamizi, vitabu, majarida, magazeti n.k., kwa kutunza sauti kwenye vyombo mbalimbali kama kinasa sauti, diski, kinyonyi, ngamizi n.k., kwa kutunza picha kwenye diski, kanda za video, ngamizi, kinyonyi n.k.
  3. Fasihi simulizi huwa na mianzo ya kifomula na miisho ya kifomula. Mianzo hiyo ni kama vile.. Paukwa…! Pakawa!, Hadithi! hadithi! , kitendawili!…… Tega!…., Hapo zamani za kale!…. n.k.
  4. Pia, fasihi hii huwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kwa hiyo fanani huwa msimuliaji au mghani. Ingawa kwa sehemu fulani fasihi simulizi husomwa lakini kiasili ni ya usimulizi wa mdomo.
  5. Usimuliaji wa fasihi simulizi huhusisha matendo ya fanani. Fanani huweza kutumia lugha ya ishara wakati wa usimuliaji. Vivyo hivyo huweza kuwahusisha hadhira kushiriki katika baadhi ya matendo kama vile kupiga makofi, kucheka n.k.
  6. Si hivyo tu, bali katika fasihi simulizi, maleba hutumika. Maleba ni mavazi ya wasanii wakiwa kwenye onyesho. Huweza kuwa, nguo za kawaida zinazoendana na tukio lifanyikalo, gunia, kofia, kinyago n.k.
  7. Mabarekebisho huwa ya papo kwa hapo. Endapo msanii atafikiri kurekebisha kazi yake, huweza kufanya wakati bado anaigiza bila kusubiri.
  8. Kwa asili yake, fanani na hadhira wa fasihi hii, huonana ana kwa ana. Kwa asili yake fanani wa fasihi simulizi husimulia akiwa na hadhira yake. Ingawa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia jambo hili halifanyiki sana. Kwa sasa fasihi simulizi huweza kuwasilishwa kwa njia ya vyombo vya habari. Kama vile redio, runinga na kwa kutumia mitandao ya kijamii.
  9. Fasihi simulizi huwa fupi na husimuliwa kwa kipindi kimoja. Hii inamaanisha kuwa masimulizi yake huanza na kuisha wakati huohuo bila kuwa na sehemu inayofuata.

Kwa ujumla fasihi simulizi ndiyo fasihi ya kwanza. Kwa hiyo, fasihi hii ilizaa fasihi andishi. Ingawa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia kuna mabadiliko makubwa ya fasihi simulizi, hasa katika uwasilishaji na uhifadhi lakini dhima za fasihi hii ni zilezile.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *