Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Lugha na Sifa Zake

Karibu tena katika mwendelezo wa makala za sarufi ya Kiswahili. Leo tutajadili kuhusu maana ya lugha na sifa zake. Kwa ujumla binadamu wote huwasiliana kwa kutumia lugha iwe ya ishara, ya mazungumzo au ya maandishi. Katika maisha ya kila siku, mwanadamu lazima atumie lugha katika kujenga jamii, kuibomoa, kuafikiana, kufarakana, kujenga uadui, kujenga uhusiano mwema, kufanya ibada n.k. Cha ajabu ni kwamba binadamu hata akiwa amelala hutumia lugha akiwa ndotoni, akihoji na kusikiliza hoja. Kwa mantiki hiyo, lugha ni chombo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.

Lugha ni nini? Wanaisimu hukubaliana kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zilizobeba maana na zilizochaguliwa na jamii fulani ili zitumike kwa makusudi ya kupashana habari au kuwasiliana. Hata hivyo, katika fasili hii tunaona kuwa kuna jambo moja muhimu linaloachwa. Jambo hilo ni ishara. Tunajua kuwa binadamu huweza kuwasiliana kwa kutumia ishara na ni kweli kuwa mawasiliano ya mwanzo kabisa yalihusisha ishara kisha sauti zilifuata. Kwa hiyo kuisahau ishara katika maana ya lugha ni kosa ambalo wanaisimu wanapaswa walitazame kwa upeo mpana. Kwa hiyo lugha ni nini? Tazama hapo chini………..

Lugha ni mfumo wa ishara au/na sauti za nasibu zenye maana na zilizochaguliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika kuwasiliana. Lugha ni muhimu sana katika jamii kwani kila jamii hujitambulisha kwa lugha yake. Kwa mfano; wamasai hujitambulisha kwa Kimasai chao, wahangaza kwa Kihangaza chao, wabena kwa Kibena chao, wajerumani kwa Kijerumani chao, waingereza kwa Kiingereza chao kwa kutaja jamii chache.

Kutokana na maana ya lugha, tunapata mambo yafuatayo yanayofasili lugha.

 1. Lugha ni mfumo wa ishara au sauti.
 2. Lugha huwa na sauti na ishara nasibu.
 3. Sauti za lugha pamoja na ishara huwa na maana iliyokubaliwa na jamii husika.
 4. Lugha humhusu binadamu aliyepo katika jamii.

Lugha ni mfumo kwa sababu sauti na ishara hupangiliwa kwa namna fulani ili ziweze kutoa maana. Pia, unasibu wa lugha hupatikana kwa sababu hapajawahi kuwa na makubaliano ya kuhusu maneno gani yatumike au ishara gani zitumike katika mawasiliano. Mambo haya yote yalitokea tu na hadi sasa yanaendelea kutokea kama ajali yaani bila ya kuwepo kwa vikao. Vivyo hivyo, ishara na sauti hizo ni lazima ziwe na maana iliyokusudiwa ili kukamilisha mawasiliano. Mwisho kabisa kwa upeo wetu, lugha ni mali ya mwanadamu kwa maana hakuna kiumbe mwingine asiye binadamu atumiaye mfumo wa lugha. Wanyama wengine hutumia milio katika kuwasiana. Hata hivyo, milio hiyo haitofautiani duniani kote. Mbwa wa Marekani hubweka sawa sawa na mbwa wa Tanzania.

Sifa za Lugha.

Kila lugha ina sifa majumui. Sifa hizo zinatajwa hapo chini.

 1. Lugha zote ni bora kwani hukidhi haja ya mawasiliano kwa jamii hisika.
 2. Lugha huweza kuathiri au kathiriwa. Hii hutokea endapo jamii zinazotumia lugha tofauti zina muwasala wa muda mrefu. Lugha za jamii hizo huweza kukopa au kutohoa maneno ya lugha nyenzie.
 3. Lugha huzaliwa, hukua na hufa. Tunajua kuwa kila lugha ilianza au ilizaliwa katika kipindi fulani. Hii ni kwa sababu hakuna binadamu aliyezaliwa na lugha. Hivyo, binadamu wa mwanzo ndio waanzilishi wa lugha zetu. Pia, lugha hukua. Kukua kwa lugha ni kuongezeka kwa misamiati ya lugha husika. Misamiati huongezeka kutokana na mahitaji ya lugha husika katika kipindi fulani. Misamiati huongezwa kwa kukopwa, kuambishwa, kutoholewa n.k. Pamoja na hayo, lugha huweza kufa endapo haitakuwa inatumiwa na jamii. Lugha mfu hapa duniani ni kama vile, Kilatini, kiebrania na lugha nyingine nyingi za kibantu zinaelekea kubeba sifa hii.
 4. Kila lugha ina mfumo wake au sarufi yake. Jambo hili linatokea kwa sababu lugha ni nasibu. Hivyo basi, mifanano inakuwa nadra sana kwani kila lugha ina sauti zake, matamshi yake, sentensi zake na maneno yenye maana zake.
 5. Lugha ni mali ya binadamu kutokana na upeo wetu. Hadi sasa hatujaweza kuthibitisha viumbe wengine watumiao lugha. Vivyo hivyo, popote alipo binadamu basi lazima pawe na lugha.
 6. Lugha zote hubeba maneno dhahania. Maneno kama vile; miungu, malaika, shetani, ndoto, n.k.
 7. Lugha zote hupoka mabadiliko kutokana na athari mbalimbali. Athari hizoni kama vile; mabadiliko ya mazingira, muwasala na lugha zingine na wakati.
 8. Binadamu yeyote huweza kujifunza lugha yoyote duniani.
 9. Lugha zote zina mfumo wa konsonati na irabu.
 10. Mwanalugha yeyote huweza kuzungumza maneno yasoukomo kwa kutumia lugha yake,
 11. Lugha yoyote huruhusu ukanushi, tasfida, unyume, visawe na matumizi ya maneno makali.
 12. Lugha yoyote huwa na kitenzi na nomino.

Kwa ujumuisho, mwanadamu hutumia lugha kama chombo kikuu cha mawasiliano. Vivyo hivyo, lugha humpa binadamu nguvu ya mawasiliano na humtofautisha na viumbe wengine. Pia, wanabaiolojia wanadai kuwa lugha ipo kwa sababu ya maumbile ya binadamu. Maumbile hayo yamefanya binadamu aweze kutamka maneno na ubongo wake ambao ni changamani unaweza kufasili maneno hayo.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *