Friday, July 10Kiswahili kitukuzwe!

Vivumishi vya Kiswahili Sanifu

Kisemantiki, kivumishi ni aina ya neno ambalo hueleza zaidi kuhusu nomino au kiwakilishi. Kwa kuwa kivumishi hueleza zaidi kuhusu aina hizo za maneno. Hivyo basi, vivumishi haviwezi kusimama katika sentensi pasina nomino au kiwakilishi.

Kimofolojia, kivumishi ni aina ya neno ambalo hujengwa na kiambishi cha upatanishi pamoja na mzizi wa kivumishi. Kwa mfano. m – zuri, ki – zuri, ki – bovu n.k.

Aina za Vivumishi

Vivumishi huweza kuwekwa katika aina mbalimbali kama ifuatavyo:

 1. Vivumishi Sifa
 2. Vivumishi Idadi
 3. Vivumishi Vioneshi
 4. Vivumishi Viulizi (vya Kuuliza)
 5. Vivumishi Vimilikishi
 6. Kivumishi Kirejeshi (Vivumishi Rejeshi)

Vivumishi Sifa

Hivi ni vivumishi viaevyoelezea zaidi kuhusu sifa ya nomino au kiwakilishi. Tazama mifano hapo chini inayoonesha aina ya vivumishi hivi:

 1. Mtoto mzuri anacheza.
 2. Kiatu kibovu hakifai kuvaliwa.
 3. Watu wema hutoa misaada kwa wasiojiweza.
 4. Mbwa ni mkali.
 5. Radio kubwa inaimba.

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vivumishi vya sifa. Pamoja na hayo maranyingi tunaona kivumishi kinaambatana na nomino au kiwakilishi chake. Hata hivyo, vivumishi ambavyo hutokea upande wa kiarifu huitwa VIVUMISHI VIARIFU ( angalia mfano namba nne) lakini hapa tutazingatia kazi inayofanywa na kivumishi hicho.

Vivumishi Idadi

Vivumishi hivi hutoa taarifa zaidi kuhusu idadi ya nomino au viwailishi vinavyozungumzwa. Tazama mifano ifuatayo.

 1. Watoto wawili wanafanya usafi.
 2. Magari manne yameongozana kwenda bandarini.
 3. Viongozi wamepitisha kanuni mbili za misitu.
 4. Wanafunzi wamelima matuta manne.
 5. Samaki wote wameliwa na makuli sita.

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vivumishi vy a idadi.

Vivumishi Vioneshi

Hii ni aina ya neno ambayo hupambanua nomino au kiwakilishi kilipo. Vivumishi vioneshi ni kama vifuatavyo;

 1. Mtoto huyu ndiye tumtafutaye.
 2. Niletee kitu kile.
 3. Matofali haya hayawezi kutosha.
 4. Simu hii imeharibika spika.
 5. Mbuzi hawa walikula mahindi ya watu.

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vivumishi vioneshi.

Vivumishi Viulizi

Hii ni aina ya vivumishi vinavyouliza kuhusu ni nomino ipi au kiwakilishi kipi kilichohusika katika jambo fulani. Tazama mifano ifuatayo kuhusu vivumishi viulizi.

 1. Mtoto yupi ni mkorofi?
 2. Wazazi wepi wanahusika na suala hili?
 3. Nyumba ipi imepata tatizo la umeme?
 4. Kwani wao waliimba wimbo gani?
 5. Aliangukia katika uwanja upi?

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vivumishi viulizi.

Vivumishi Vimilikishi

Hivi ni vivumishi vnavyoonesha nomino au kiwakilishi kinamiliki nini. Tazama mifano ifuatayo.

 1. Mtoto wangu amenitembelea.
 2. Kiatu chake ni kizuri sana.
 3. Nchi yetu inapiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
 4. Umeme wa jenereta hauna nguvu kubwa.
 5. Sikuisikia sauti yake mahala popote.

Maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vuvumishi vimilikishi.

Vivumishi Rejeshi

Hivi ni vivumishi ambavyo vinarejelea nomino au kiwakilishi tajwa. Tazama mifano ifuatayo kwa maelezo zaidi.

 1. Kiatu chenyewe hakijapakwa dawa.
 2. Mtu mwenyewe hana hata nguvu.
 3. Shule yenyewe haina umeme.
 4. Leo ndiyo siku yenyewe.
 5. Jamaa mwenyewe ndiye yule palee!

maneno yaliyoandikwa kwa herufi mlalo ni vivumishi rejeshi.. Tumeita vivumishi rejeshi na si vya pekee kama mahala pengi waviitavyo, ili kuondoa utata uliopo katika neno pekee. Kwa namna fulani neno pekee huhusisha sifa za kipekee ambazo huwezi kuzipata katika mahala pengine. Upekee tunaukuta zaidi katika nomino (kwa maarifa zaidi kuhusu nomino za pekee na sifa zake tafadhali rejea katika mada ya kwanza inayohusu Nomino za Kiswahili Sanifu).

ANGALIZO

Hatukujadili kuhusu kivumishi cha a-unganifu kwa sababu ni ukweli kwamba hakuna kivumishi cha namna hii. Sehemu zote zinazojadili kuhusu kivumishi cha namna hii huchanganya na dhana au kazi ya kuhusishi. Pia, kwa namna fulani sehemu hizo hazijadili kabisa kuhusu aina hii ya neno ingawa ni aina ya msingi sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *