Monday, April 12Kiswahili kitukuzwe!

Fasihi Kwa Ujumla

Karibu katika sehemu hii ya mjadala kuhusu fasihi. Kwa ujumla fasihi ni miongoni mwa sanaa zisizoweza kutengwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Fasihi huweza kutokea wakati wa sherehe, misiba, tambo, kazi za msarambo (zile zinazofanywa kwa kushirikiana), wakati wa kutoa maonyo na majuto. Kutokana na mambo hayo yote inaonekana kuwa fasihi na maisha ya mwanadamu ni kama pande mbili za shilingi. Hata hivyo, fasihi ni nini? swali hili linajibiwa hapo chini.

Fasihi ni sanaa itumiayo lugha katika kufikisha ujumbe wake. Fasihi ni sanaa kwa kuwa hutumia ufundi katika kuwasilisha ujumbe kwa hadhira. Ufundi huo huonekana zaidi katika matumizi ya lugha ambapo lugha za kisanaa hutumika. Lugha hizo ni kama vile; mbaalagha, taswira, ishara, matumizi ya semi, nidaa, tashibiha, takriri, tashititi, taniaba, tabaini na kejeli kwa kutaja chache. Pia, ufundi wa kifasihi huweza kuonekana katika matumizi na uteuzi wa wahusika, mandhari, mtindo na muundo wa kazi yenyewe. Ufundi wote huu hutumika ili kuburudisha na kuelimisha jamii husika.

Dhima za Fasihi

Fasihi ina kazi zifuatazo katika jamii.

 1. Fasihi huelimisha jamii kutokana na dhamira zinazopatikana katika kazi nzima ya fasihi. Dhamira hizo huweza kuonesha mathara ya rudhwa, ulevi, ukiukwaji wa maadili n.k. Haya yote humsaidia hadhira kutafakari upya kuhusu yatokeayo katika jamii yake.
 2. Fasihi huburudisha jamii kwa kutumia wahusika, miundo, mtindo na matumizi ya lugha. Vipengele hivyo hutumia usanaa ili kumburudisha msomaji huku akipokea ujumbe kusudiwa,
 3. Fasihi hutunza amali za jamii kama vile; mila, desturi, imani na itikadi. Amali hizi hutunza kwani msanii huandika mambo yote yanayoizunguka jamii. Kwa kuwa mambo hayo huandikwa ni vigumu kupotea kizazi hadi kizazi.
 4. Fasihi hutunza historia ya jamii pale ambapo matukio mbalimbali ya kihistoria yatakapohifadhiwa kwa fasihi. Kwa mfano, tarihi, riwaya za tawasifu na riwaya za wasifu hueleza mambo ya kweli yaliyotokea katika kipindi fulani. Vivyo hivyo, fasihi huweza kuonesha jamii ilipotoka kiitikadi, kiimani na kimsimamo hivyo historia ya jamii hiyo kutunzwa.
 5. Fasihi hukuza lugha kwa wajifunza lugha hata wamilisi wa lugha husika. Fasihi inasifika katika kuongeza misamiati kwa wajifunza lugha kwani inatumia lugha ya kila siku. Vivyo hivyo umahiri wa lugha huongezeka kwa wasoma au waandika mashairi hasa ya kimapokeo.
 6. Huonesha ukweli kuhusu maisha kwani kwa kupitia fasihi msanii huweza kuzungumza mambo mengi zaidi tena bila woga. Mambo hayo ni mambo yanayotokea kila siku katika maisha ya mwanajamii. Yanayochukiza au yanayofurahisha, yanayojenga au yanayobomoa, yanayounganisha au yanayotenganisha na yanayohamasiha au yanayokatisha tamaa.
 7. Huendeleza harakati katika jamii kwa uonesha ni kwa namna gani tabaka fulani hukandamizwa na tabaka lingine. Kwa hiyo harakati hizo huweza kuwa za ukombozi, uwajibikaji, elimu n.k
 8. Hujenga utaifa kwa kuonesha namna umoja wa kitaifa ulivyo na faida na kuhimiza ushirikiano bila kujali tofauti za kimila, kiitikadi, kidini, rangi wala kikabila.
 9. Hujenga tabia mbalimbali na mara nyingine hubadilisha tabia ya hadhira kwa kiasi kikubwa. Kama hadhira husoma mara kwa mara hadithi za kutisha, mtu huyo huweza kujenga tabia ya woga. Lakini kama atasoma hadithi za kishujaa mara kwa mara, hadhira huweza kuwa jasiri na hodari.

SIFA ZA FASIHI

Kuna sifa mbalimbali za fasihi ambazo huweza kuitofautisha fasihi na kazi zaingine za kisanaa. Sifa hizo ni kama zifuatazo;

 1. Huwakilishwa kwa njia ya maandishi au ya masimulizi ya mdomo.
 2. Hutunzwa kichwani, kwenye maandishi, kwenye kompyuta (ngamizi), makumbusho, kwenye kanda za video n.k.
 3. Huwa na pande mbili ambazo ni upande wa fanani (watunzi/waandishi) na upande wa hadhira (wasomaji).
 4. Hupokea mabadiliko yawe ya papo kwa hapo au ya kusubiri toleo lingine.
 5. Humilikiwa na jamii nzima au na mwandishi pekee.
 6. Hutumia lugha iwe ya maandishi au ya masimulizi ili kufikisha ujumbe wake.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *